Udhaifu wa sayansi (1)

Haya tuendelee.

Tunahitaji aya nyingi kufafanua dhana ya sayansi. Kwanza nijitete kwamba sina msamiati wa kutosha kukwepa maneno yanayoitwa ya kisayansi ila nitajaribu kadiri niwezavyo.
Kwa uchache sana, na katika lugha rahisi zaidi, sayansi ni namna ya upatikanaji wa maarifa kwa njia ya utafiti. Utafiti hapa humaanisha majaribio ambayo hukusudiwa kuchunguza na hatimaye kuthibitisha ama kukanusha bashiri ya kisayansi.

Sayansi hutumia mbinu katika kuchunguza dhana, ili kuongeza maarifa ama kurekebisha maarifa yaliyopo. Huanzia katika ukusanyaji wa ushahidi unaochunguzika, unaopimika, na wenye chanzo mahususi kinachokubaliana na ufahamu wa kawaida. ( Sina masamiati sahihi sana).
Ushahidi huo, ndio kile kinachoitwa data, ambazo hupatikana kwa majaribio ambapo bashiri hujengewa hoja ili kufanyika maelezo ya dhana iliyokuwa ikichunguzwa. Majaribio haya hupangiliwa kitaalamu kwa kutumia vibadiliko (variables) ili kuzijaribu bashiri za awali.
Majaribio haya hufanyika katika mazingira ambayo yamedhibitiwa ili kuhakikisha kuwa kisababishi cha matokeo yanayopatikana kinajulikana wazi pasipo shaka. Hapo hupatikana kile kinachoitwa nadharia ya kisayansi.

Ikiwa nadharia hiyo itathibitishwa na watu kadhaa kuwa kweli, basi hapo nadharia hiyo hupanda hadhi na kuwa kanuni rasmi ya kisayansi.

Sayansi pia imegawanyika katika vipengele vingi ambavyo sitavijadili angalau kwa sasa.
Pamoja na uzuri wake, sayansi inayo mapungufu mengi. Mara nyingi sayansi hufanyika kwa njia ya majumuisho kwamba matokeo yaliyopatikana katika mazingira fulani (kwa hali fulani iliyokuwapo) hutumika kuelezea hali nyinginezo ambazo pengine hazikujumuishwa katika jaribio hilo. Njia hii huitwa inductive reasoning ( Bakita mpo?). Tatizo linalojitokea ni kwamba si mara zote matokeo haya hufanana katika mazingira mengine na katika mukhtadha mwingine. Huu kwangu ni udhaifu nitakaoutolea mifano mbeleni.

Lakini pia, ni wazi kuwa wanasayansi wengi huwa na nadharia zao vichwani kabla hata ya kufanya majaribio yenyewe. Kwa lugha rahisi, watu hawa hupangilia majaribio yao ili kutetea hitimisho ambalo mara nyingi hufanyika kabla. Kwa maneno mengine, kile kinachitwa testing the theory ni kiini macho kwani ni kutafuta tu mashikio ya kitu amabcho kimeshakuwepo kichwani mwa mtafiti.
Ionekanavyo ni kwamba sayansi husimamia katika mawazo ama bashiri za watu. Bashiri hizi huweza kuwa mazao ya matakwa binafsi ya mwanasayansi mwenyewe. Mawazo haya huweza kufanyiwa kazi kwa 'kucheza na matokeo ya utafiti' katika jitihada za kujaribu kushawishi usahihi wa mawazo hayo. Habari (data) huchaguliwa kwa kuangalia namna zinavyokubaliana na mawazo ya mtu ajiitaye mwanasayansi zaidi kuliko hali halisi. Matokeo yake, huzaa nadharia ambazo huweza kushawishi ukubalikaji wake katika jumuia za kisayansi.

Tunaweza kulithibitisha hili kwa kuangalia ukweli mmoja. Zipo nadharia nyingi ambazo zilipata kuwapo na kutamba sana miongoni mwa wanasayansi, lakini baada ya muda, nadharia hizo zilipigwa teke kwa kutumia matokeo ya tafiti zilizopindishwa kidogo na wanasayansi wengine. Ukanwaji wa nadharia hizi hufahamika kama paragim shift, uthibitisho kuwa sayansi haiishi kigeugeu.

Aidha, umaarufu anaokuwa nao mwanasayansi pamoja na umbumbumbu wa jamii alimo, hurahisisha kwa kiasi kikubwa upokelewaji wa matokeo yaliyopikwa mithili ya kura za uraisi katika nchi nyingi za Kiafrika. Mara zote, jamii imekuwa iliyapokeo hayo yanayoitwa mapendelkezo ya wanasayansi bila maswali kwa kuamini kuwa hawa ni binadamu wasiokosea. Hapa sizungumziii watu wale wanaitwa wa kawaida, bali hata hawa wanaojisifu kuwa eti ni wanataaluma.

Mfano leo hii, James Watson, yule jamaa aliyevumbua kiasili kiitwacho DNA, uvumbuzi uliomfanya aogelee kwenye sifa zinazomzidi, akija na tamko lolote la kijinga, bila hata ushawishi wa kisayansi, nina hakika tamko hilo halitakumbana na upinzani wa maana katika ulimwengu uitwao wa wanasayansi acilia mbali ule mwingine uitwao wa watu wa kawaida.


Vile vile, kwa sababu ya kuhitaji zaidi ukusanyaji wa taarifa kwa kutumia majaribio rasmi, sayansi inayo mipaka yake katika ufanyaji kazi. Yapo maeneo mengi ambayo hayaelezeki kwa lugha ya kisayansi, na wala hayathibitishiki kwa kanuni za kisayansi ingawa maeneo hayo ni halisi. Nitatoa mifano baadae.

Niishie hapo, kwa kukuomba mawazo yako wakati najiandaa kukuletea mifano halisi ya haya ninayojaribu kuyaweka hapa.

Samahani kwa mwandiko wa mcharazo nimeandika kwa haraka sana na sikuwa na muda wa kuhariri kazi ambayo nakuachia mwenyewe.

Nakutakia mwisho mwema wa mwezi.

Maoni

  1. Mwandiko wako wa mcharazo unasomeka na kueleweka:-)

    JibuFuta
  2. Nadhani ni kwa sababu umeuzoea. Asante kwa kutembelea kibanda hiki Simon!

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Uislamu ulianza lini?