UmahiriHisia (Emotional Intelligence) Unavyochochea Motisha na Kujituma

Kuna kukosa ari ya kaza. Msimamizi wako asipokufuatilia na kuweka utaratibu wa kukudhibiti ufanye unachopaswa kufanya, hakuna unachoweza kuonesha kama matokeo. Huna msukumo wowote wa kujituma na wala hujisikii hatia.

 

Hali kama hii inaweza kusabishwa na mengi. Kuna suala la mazingira magumu ya kazi. Hupati vitendea kazi unavyohitaji ili kufanya kazi yako vizuri. Kuna suala la uongozi usiojali hisia zako. Unalalamika na hakuna anayeonekana kusikia. Kuna  mengi yanayoweza kukufikisha mahali ukapoteza motisha ya kazi. 

 

Wengi wanaposikia motisha wanawaza matokeo mazuri unayopata aghalau kutoka kwa mtu kama kichocheo cha kufanya kazi. 

“Hapa hatupewi motisha yoyote.”

 “Tunafanya kazi na hakuna motisha.”

“Toeni motisha muone nitakavyofanya kazi.”

 

Tunapozungumzia motisha hatuzungumzii kutambuliwa kwa kazi unayofanya, kuonekana, kusifiwa, kupandishwa cheo wala kupewa kitu kama bakhshishi ya bidii yako ya kazi. Motisha ni ile sababu inayoamsha ari ya kujipata, kujua unataka kufanya nini na maisha yako, kubaini na kupambania malengo uliyonayo. Motisha ni ule msukumo unaomnyima mtu usingizi ili atie bidii kwenye kile anachokifanya. 

 

Motisha huleta nidhamu. Mtu mwenye motisha ana uwezo wa kusema hapana kwa chochote kinachoingilia malengo. Nikisema nina nidhamu maana yake ninaweza kusimamia malengo yangu kwa kujijengea utaratibu wa maisha yanayotabirika kuwezesha kutekelezeka kwa malengo hayo.

 

Kiwango cha juu kabisa cha nidhamu hufikiwa unapoweza kupangilia muda wako na namna unavyoutumia bila kusubiri kuendana na mwelekeo wa upepo wa siku. Nidhamu ya kiwango hiki inategemea uwezo mkubwa wa kumudu hisia zako, namna unavyonyamazisha matamanio yako, na kuchochea ari ya kulipa gharama ya kesho iliyobora. 

 

Walter Mischel, mshunuzi maarufu aliyepata kuwa pia mwalimu wa Chuo Kikuu cha Stanford nchini Marekani alifanya utafiti unaoendelea kuthibitika duniani kote kuonesha kuwa siri ya mafanikio ya mtu ni uwezo wake wa kudhibiti mihemuko (tamaa ya macho, hisia) kama gharama ya kufikia małengo. 

 


Mischel aliwatumia watoto wa miaka minne, wengi wakiwa watoto wa walimu wa chuo hicho. Kawagawia wale watoto, mmoja mmoja kwa wakati tofauti Marshmallow, mfano wa keki tamu zinazopendwa na watoto wa Kimarekani. Mischel anawapa maelekezo rahisi, “Kaa hapa na Marshmallow naondoka kidogo. Ukiweza kusubiri nikirudi ukawa hujaila nikaikuta, basi nitakupa ya keki ya pili.” Marshmallow ya pili ilikusudiwa kuwa ‘zawadi ya ushindi’ kwa maana ya kuutambua uvumilivu wa mtoto. 

 

Hata hivyo, ikiwa mtoto angeila, haidhuru, lakini mtoto asingepata zawadi ya keki (marshmallow) ya pili. Mischel anaondoka baada ya kuhakikisha mtoto ameelewa maelezo hayo, anarudi baada ya dakika kumi na tano.

 

Unadhani watoto wangapi walivumilia? Watatu kati ya kumi ndio walioweza kusubiri. Saba kati ya kumi kusubiri ulikuwa mtihani mgumu sana. Kwa hawa saba, ilionekana bora kula ulichonacho wakati huo kuliko ahadi isiyo na uhakika. 

 

Mischel hakuishia kwenye Marshmallow. Kawatia alama watoto bila wao kujua, kisha akawafuatilia kwa miaka kadhaa kujua wanaendeleaje shuleni, ule umri korofi wa ujana chipukizi wanaupitaje, ujanani mapenzi yanawapelekaje, nidhamu ya fedha, na kadhalika na kadhalika. 

 

Hili Mischel hakulitarajia. Wale watoto walioweza kuutumia uhuru wao vizuri na kuchagua kuvumilia kukaa na keki tamu wasiile, ndio walifanya vizuri shuleni, ule umri korofi hawakuwa na matatizo mengi na hata kwenye sekta ya mapenzi hawakuwa na maumivu mengi. Walioshindwa kusubiri, ambao ndio wengi, Mischel kagundua, walikuwa na matatizo mengi shuleni, ufaulu hafifu, nidhamu mbovu ya fedha, majeraha ya kutosha kwenye mahusiano na hata bangi haikuwapita. 

 

Mischel akawa amegundua kanuni ya kishunuzi (psychology) kubashiri mustakabali wa mtu. Kwamba, uwezo wa kumudu mihemuko unatafsiri maana ya nidhamu na ndiyo nyenzo muhimu ya mafanikio. Uwezo wa kujizuia huamua utafika umbali gani. Ukishindwa kuwa mtu unayejizuia kwa shauku za muda mfupi, utapata shida na mambo mengi kwenye maisha. Hata fedha ni nidhamu inayoanza na uwezo wa kupumzisha matakwa ya ghafla ghafla kwa faida ya kesho. Tunarudi mule mule kwa Mischel. Usile Marshmallow yako.

 

Kadhalika, huwezi kujizuia ikiwa hujaweza kuyaona matokeo kabla hayajatokea. Mischel alibaini kuwa watoto walioweza kuushinda mtihani wa kujizuia walikuwa na uwezo mkubwa wa kuona matokeo ya nidhamu hiyo. Uwezo huu wa kuona matokeo kabla hayajatokea ndio uliowatofautisha watoto wenye nidhamu na wenzao waliofanya maamuzi kwa kuzingatia kile wanachokiona. Ndio kusema kujiwekea malengo kunaanza na uwezo wa kuona matokeo. 

 

Aidha, nidhamu ni imani anayokuwa nayo mtu kwa mamlaka. Watoto waliojizuia, kwa mfano, walikuwa na imani na Walter Mischel kwamba angetimiza ahadi yake. Kwa nini wengine hawakuwa na imani naye, hilo linategemea mengi. Lakini kwa mazingira yetu inawezekana isiwe kuwa na imani bali kutii hata kama ni kwa hofu ya kuogopa adhabu. Utafiti kama huu ulifanyika Cameroon na matokeo yalionesha kuwa watoto wa ki-Cameroon walikuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kusubiri kuliko watoto hawa wa utafiti wa Michel. Hata kama pengine waliogopa adhabu ya kwenda kinyume na maagizo lakini ni wazi walikuwa na subira.  

 

Kubwa tunalojifunza, hata hivyo, nafasi ya malezi katika kujenga subira. Unapokuwa na mtu mwenye raslimali (ujuzi, uzoefu, hekima) anayeweza kutoa mwongozo unaorahisisha ufikiwaji wa malengo inakuwa rahisi mtoto kujifunza kulipa gharama ya kuwa na subira. Huyu anaweza kuwa mzazi, mwalimu, mchungaji, sheikh au kiongozi mwingine.

 

Utafiti huu unatufundisha namna nidhamu inavyojengwa. Tunaona watoto wenye nidhamu, Mischel anaeleza, ni wale waliokuwa na uwezo wa kufikiri matokeo ya nidhamu. Mtoto aliyeweza kuvuta picha ya kupata pipi ya pili alikuwa na nidhamu zaidi ya mwenzake ambaye hata picha haikumjia kichwani.  

 

Uwezo huu wa kufanya kitu bila kusubiri ‘presha’ ya nje au msukumo wa matarajio ya watu ndio unaoonesha kuwa mtu ana umahirihisia. Kwa nini? Mtu huyu ana uwezo wa kujiwekea malengo, kuona matokeo ya kazi anayofanya, kujiwekea mazingira yanayowezesha malengo hayo kufikiwa na kisha kujikumbusha mara kwa mara kwa nini anafanya kazi anayoifanya. Unapokuwa na msukumo mkubwa wa kiwango hiki maana yake hukosi kuwa mtu anayejituma katika kazi.

 

Motisha, kwa kawaida, hukuongezea msukumo wa kujenga umahiri na uwezo wako wa kazi unazofanya. Umahiri nao, kwa upande mwingine, huleta utoshelevu. Ukishakuwa na utoshelevu kuna namna unajisikia kuridhika hata kama bado una safari ya kupambania malengo makubwa uliyonayo. Utoshelevu huambatana na matumaini kuwa kesho itakuwa bora zaidi. Utoshelevu huambatana na mtazamo chanya kuwa, hata unapopita kwenye mitihani ya maisha, bado utatoka salama. 

 

Hali hii ya utoshelevu ndiyo inayokufanya uone bado unawajibika kuchukua hatua badala ya kuwalaumu wengine. Habari njema kuhusu utoshelevu ni namna unavyokufanya ujisikie fahari bila kumtia unyonge asiye na uwezo huo. Hisia hizo za ufahari hutukumbusha thamani yetu mbele ya jamii na bado zikaweza kutusukuma kuwatia ujasiri hata wale tunaowazidi.

 

 

Kufanyia kazi unachojifunza

 

Ukiwa na motisha, ni wazi utakuwa na matumaini. Ukiitazama kesho yako unauona uwezekano badala ya mkwamo. Huwi mlalamishi badala yake unakuwa mtu anayewaza zaidi majibu ya changamoto zilizopo. Huwatupii wengine lawama na badala yake unajirudishia wajibu wa kufikiri wapi ungeweza kuwajibika zaidi. 

 

Hata pale unapoona jambo haliendi vyema, unaweza kutafuta namna bora ya kuzungumzia mapungufu yake bila kumshambulia mtu na kutweza utu wake. Nikuulize, mara ngapi umemshambulia mtu kuficha hali yako ya kukataa tamaa? Umewasengenya wangapi ambao, kama ungewajibika kidogo, pengine ungewasaidia bila kuwachafua kwa maneno na vitendo?

 

Unakumbuka tukio lolote unaloweza kusema linaonesha hali ya uvivu, kwa maana ya kutokuwajibikia jambo pasipo msukumo wa nje? Umewahi kujisikia kupoteza ari ya kazi unayofanya? Unahusishaje hali hiyo na umahirihisia? Huenda umeshindwa kurekebu hisia zako kwa  wakati, na matokeo yake, zimekugeuza kuwa mtumwa wa historia yako, kushindwa kwako, badala ya kukujaza ujasiri wa kupambana na kesho iliyobora zaidi.

 

 

 

Maoni

  1. Ubarikiwe sana kk. That is the good things to be learnt.

    JibuFuta
  2. Asante mwalimu wangu wa ushunuzi.Nimekuwa mtumwa wa tamaaa za maisha kwa kutaka matokeo ya haraka kiasi kwamba nimepata maumivu mengi sana katika jana wangu huu kwa kupoteza fedha nyingi sana.Nipo nachukua hatua ili nizimudu hisia zangu na nice na subira

    JibuFuta
  3. Baada ya kuwa na uhusiano naye kwa miaka saba, aliachana nami. Nilijaribu kila niwezalo kumrudisha lakini yote yalikuwa bure. Nilitamani arudi vibaya sana kutokana na mapenzi niliyonayo kwake na nilimsihi kwa moyo wangu wote, nilimpa ahadi lakini alikataa. Niliwasiliana na mganga aitwaye DR Dawn, ambaye angeweza kunisaidia kuniroga ili kumrejesha lakini mimi ni mtu ambaye sikuwahi kuamini uchawi, sikuwa na jinsi zaidi ya kujaribu. Nilimtumia barua pepe mganga huyo na akaniambia kwamba hakuna tatizo lolote, kwamba kila kitu kitakuwa sawa baada ya siku mbili na kwamba mpenzi wangu wa zamani angerudi kwangu baada ya siku tatu. Alipiga uchawi na cha kushangaza, siku ya pili, ilikuwa karibu 4:00 PM. Mpenzi wangu wa zamani alinipigia simu, tukasuluhisha tofauti zetu na sasa tuna furaha pamoja. Yeyote anayeweza kuhitaji usaidizi wa mtangazaji huyo anaweza kumtumia barua pepe kwa ( dawnacuna314@gmail.com ) au /WhatsApp kwa: +2349046229159

    Kwa uchawi wa kuungana tena.
    Kwa ujanja wa ujauzito.
    Kushinda bahati nasibu.
    Kushinda kesi mahakamani.
    Mimea ya kutibu, kila aina ya magonjwa kama,
    VVU UKIMWI Kansa malengelenge na zaidi.

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Uislamu ulianza lini?

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Haiba ni nini?

Kama sio utumwa ni nini hiki?

Kuanzisha na Kuimarisha Urafiki wa Karibu