Mambo ya Kuzingatia Unapompeleka Mwanao Kwenye Kituo Cha Malezi

Watafiti wa malezi ya watoto wamejaribu kuangalia namna gani huduma za malezi ya kituoni –day care yanavyoweza kuboreshwa. Moja wapo ya watafiti maarufu katika eneo hili ni Taasisi ya Marekani ya Mtandao wa Afya ya Mtoto na Maendeleo ya Utafiti wa Malezi ya Watoto (NICHD).

Maswali ya msingi yanayojaribu kujibiwa na tafiti hizi ni ikiwa kuna uhusiano wa ubora wa huduma zinazotolewa na vituo hivi na makuzi ya mtoto katika nyanja za kiakili, kihisia, kimwili na kistadi; aina ya mazingira yanayoweza kuhusianishwa na ukuaji mzuri wa kihisia na kiakili kwa mtoto na kiasi cha masaa kinachopendekezwa kwa mtoto kulelewa katika kituo kwa siku/juma.

Jambo lililodhahiri ni kuwa huduma hizi zinapoboreshwa hupunguza uwezekano wa changamoto zinazotokana na huduma zisizokidhi viwango. Makala haya yanaangazia vigezo vilivyothibitika kusaidia kuondoa kwa kiasi kikubwa madhara hayo kwa makuzi ya mtoto.


Uwiano wa idadi ya walezi na watoto

Idadi ya watoto wanaoangaliwa na mlezi (mwalimu) mmoja ni muhimu. Ingawa zaweza kuwepo tofauti za kiutamaduni baina ya nchi na nchi, kwa ujumla tunaweza kusema ni vyema watoto wadogo waangaliwe kwa ukaribu zaidi wanapokuwa kituoni.

Kwa mujibu wa NICHD, watoto wenye miezi 6 hadi mwaka 1½, kwa mfano, uwiano wapaswa kuwa angalau watoto watatu wanaoangaliwa na mlezi mmoja. Kwa mwaka 1½ mpaka 2 uwiano unaopendekezwa ni watoto watano kwa mlezi mmoja, na kwa miaka 2 mpaka 3, uwiano unaopendekezwa ni watoto saba hadi kumi kwa mlezi mmoja.

Watafiti wengine wanashauri kwa umri usiofikia miezi sita, ni vizuri kila mtoto awe na mlezi wake. Lengo la uwiano huu ni kuwasaidia watoto kupata uangalizi wa karibu unaozingatia mahitaji binafsi ya kila mmoja.

Ukubwa wa makundi ya watoto

Ukubwa wa kituo cha malezi nao ni kigezo kimoja wapo cha ubora wa huduma. Inapendekezwa kuwa watoto wawekwe kwenye makundi madogo yanayoangaliwa na walezi zaidi ya mmoja ili kuwawezesha kufahamiana kwa karibu.

Kufahamiana kunawasaidia kuwapa utulivu wa kisaikolojia na kuwapa fursa walezi kushirikiana kwa karibu katika kuwasaidia watoto.

Kwa mtoto mwenye  miezi 6 hadi mwaka 1½ inapendekezwa watoto sita wawe kwenye kundi mmoja, wakiangaliwa na walezi wawili. Mwaka 1½ mpaka 2, watoto nane kwa kundi, wakiangaliwa na walezi wawili.

Tafsiri ya mapendekezo haya katika mazingira yetu, ni kuwa kituo kinahitaji kuwa na walezi wa kutosha kuwaangalia watoto kwa karibu. Hili linawezekana ikiwa kituo unachofikiri kumpeleka mwanao kitakuwa kimesajiliwa na mamlaka zinazohusika.
 
Mafunzo kwa walezi
 
Ubora wa kituo pia unategemea ubora wa mafunzo waliyonayo walezi. Inashauriwa walezi wawe wamejifunza angalau mambo ya msingi kuhusu makuzi. Mafunzo hayo yatawasaidia kujua namna ya kufanya kazi na watoto kwa kuzingatia mahitaji yao maalum.

Katika nchi yetu, tunavyo vyuo vinavyotoa mafunzo ya elimu ya awali kwa ngazi ya Astashahada, Stashahada na hata Shahada. Ni muhimu kuwatumia walimu hawa kufanya kazi ya kuwalea watoto katika vituo hivi.

Walezi wanapokuwa na uelewa wa mahitaji ya watoto, watakuwa kwenye nafasi ya kujua aina ya vifaa vinavyowasaidia watoto kujifunza kulingana na mahitaji yao; aina ya michezo inayowafaa watoto na mambo kama hayo.

Mazingira rafiki na salama kwa mtoto

Inashauriwa kituo kiwe na mazingira rafiki yanayomfanya mtoto ajisikie salama. Hiyo ina maana ya kuhakikisha kuwa walezi wanao uwezo wa kujenga mahusiano mazuri na watoto; hawabadiliki kila mara kwa lengo la kuwaondolewa watoto kadhia ya kukutana na sura ngeni mara kwa mara.

Pia, nyumba/jengo linalotumiwa kwa huduma ya malezi lisiruhusu mtoto kutoka bila uangalizi. Lengo ni kuhakikisha kuwa muda wote mtoto anabaki salama ndani ya jengo isipokuwa kwa uangalizi wa mlezi.

Usalama pia unakwenda sambamba na kupatikana kwa huduma bora za usafi na chakula, malazi safi, michezo na vifaa muhimu vya mtoto kujifunzia kulingana na umri.

Masaa ya mtoto kubaki kituoni

Tafiti nyingi zilizofanyika katika nchi zinazoendelea zinabainisha kuwa upo uhusiano wa moja kwa moja kati ya muda mrefu anaoutumia mtoto kituoni na kuzorota kwa uhusiano wake na wazazi.

Kwa mfano, mtoto chini ya mwaka mmoja anapoachwa kwa zaidi ya masaa sita kwa siku anaweza kujenga tabia hasi kama upweke na kukosa imani na wazazi. Ingawa hatuna tafiti zilizofanyika kwenye mazingira yetu, ni dhahiri kuwa upo umuhimu wa kupunguza muda wa kumwacha mtoto kituoni.

Hata hivyo, kadri mtoto anavyoendelea kukua, muda anaoweza kuachwa mtoto kituoni unaweza kuongezeka. Pamoja na hayo, ni vyema kuhakikisha kuwa mtoto anakaa muda mfupi iwezekanavyo kituoni sambamba na jitihada za kujenga uhusiano mzuri na mtoto mara baada ya kuondoka kituoni.

Hitimisho


Tunaweza kuhitimisha kuwa huduma hizi za malezi nje ya nyumba zetu, zinaweza kufaa. Jambo lililo muhimu kuzingatia ni ubora wa huduma zinazotolewa kwenye vituo hivi.

Katika jitihada za kuhakikisha kuwa vituo hivi vinaendeshwa kwa ubora, ni muhimu kwa mamlaka zinazohusika kuhakikisha kuwa vituo hivi vinasajiliwa. Wafanyabiashara wanaoanzisha huduma hizi walazimike kutumia majengo yenye ubora, wawe na vifaa muhimu vya michezo na waajiri walezi wenye mafunzo yanayotambuliwa.


Vile vile, tunahitaji sera za kazi za ajira zinazowezesha akina mama kufanya majukumu yao ya kimalezi bila changamoto kubwa. Kwa mfano, kuongeza muda wa likizo ya uzazi anayopewa mfanyakazi wa kike anayejifungua inaweza kusaidia kupunguza changamoto nyingi za malezi. 

Fuatilia Safu ya Uwanja wa Wazazi kwenye gazeti la Mtanzania kila Alhamisi kwa makala kama hizi.

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Pay $900? I quit blogging

Heri ya mwezi mpya!