Hatua za Kuchukua Unapoamua Kuacha Kazi -1

Kuacha kazi si jambo dogo. Lakini zipo sababu kadhaa zinazoweza kukufanya uamue kuacha kazi. Mosi, kupata kazi mpya. Unapoitwa kuanza rasmi kazi uliyoomba, ni vigumu kuendelea na kazi uliyonayo. Kwa kuwa ni vigumu kuwa na ajira mbili kwa wakati moja, mara nyingi utalazimika kuacha kazi uliyonayo.

Pia inawezekana umeshindwa kuendelea na kazi uliyonayo hivi sasa. Ingawa haishauriwi kuacha kazi bila kuwa na uhakiki wa kazi nyingine, hutokea mtu akafikiri kwa kina, akapata ushauri wa kitaalam na kujiridhisha kuwa ugumu wa mazingira ya kazi haumruhusu kuendelea na kazi aliyonayo.

Mathalani, kutokuelewana na mkubwa wako wa kazi au wafanyakazi wenzako; kutokuridhika na tija ya kazi unayoifanya; kukosa motisha na ari ya kazi; kujihisi huna mchango tena ofisini kwako ni baadhi ya sababu zinazoweza kusababisha maamuzi magumu ya mtu kuacha kazi.

Lakini pia inawezekana ukalazimishwa kuacha kazi hata kama bado ungependa kuendelea nayo. Kama ambavyo mwajiriwa anaweza kuamua kuacha kazi, mwajiri naye anaweza kuamua kukuachisha kazi kwa sababu anazoona zinafaa.

Vyovyote vile iwavyo, tukio la kuacha kazi si jambo jepesi.  Makala haya yanalenga kujadili hatua unazoweza kuchukua mara unapoamua kuachana na kazi yako iwe kwa hiari au kwa kulazimika.




Tafuta ushauri unaoaminika

Usiache kazi kwa sababu tu unafikiri huhitaji kuendelea kufanya kazi uliyonayo sasa. Mazingira magumu ya kazi yanaweza kukushawishi kufanya maamuzi utakayoyajutia baadae. Inawezekana huna mahusiano mazuri na mkubwa wako wa kazi. Unafikiri kuacha kazi ni kumkomoa na kulipa kisasi.

Inawezekana unafanya kazi katika maeneo usiyoyapenda. Unafikiri ukienda kwingineko mambo yatakuwa mazuri. Pengine umevutiwa na mwajiri mwingine anayeahidi kukuongezea mshahara zaidi.  Lakini hujafikiria kuwa mwajiri wa sasa anayekulipa kidogo, anakupa uhuru wa kufanya mambo mengine yanayoweza kukuongezea kipato. Huko unakokwenda unaweza usipate muda wa kufanya mambo hayo. Msisimuko wa kupata kazi unayoipenda unaweza kukufanya ukasahau kufikiria mambo ya msingi yanayoweza kukugharimu baadae.

Kabla hujatekeleza azma yako, fanya mawasiliano na watu  wasio na maslahi na kazi yako na wenye uzoefu zaidi yako. Watu hawa watakusaidia kuyatazama mambo kwa mtazamo mpana. Ushauri wao unaweza kukufanya ugundue kuwa huna sababu ya kuacha kazi uliyonayo isipokuwa kuangalia namna ya kutatua changamoto ulizonazo hapo ulipo.


Aidha, inawezekana unaacha kazi kwa sababu umelazimika kufanya hivyo na mwajiri wako. Kuacha kazi katika mazingira haya kunaweza kuambatana na maumivu makubwa. Hisia za kuonewa na taasisi au kampuni inayomlazimisha kuacha kazi; hofu ya aina ya maisha atakayoishi baada ya kuacha kazi;  wasiwasi wa kukosa hadhi aliyokuwa nayo kama mfanyakazi ni baadhi ya sababu zinazoweza kumfanya mtu aache kazi kwa moyo mzito.

Unahitaji kuonana na watalaam wa unasihi wakusaidie kuchukuliana na taarifa hizi. Wakati mwingine, huhitaji ushauri wowote zaidi ya watu wakomavu unaowaamini watakaokusikiliza tu. Wape nafasi kabla hujachukua hatua zozote.

Onyesha utulivu wa kihisia

Inawezekana umepata kazi nzuri yenye maslahi makubwa zaidi. Furaha hiyo isikufanye ukakosa busara. Inawezekana mwajiri wako alikunyima haki zako kinyume na makubaliano yenu ya kazi.  Unaweza kuchukulia kupata kazi mpya kama namna fulani ya kutoka kifungoni. Hiyo haiwezi kuwa sababu ya kutosha kukunyang’anya hekima.

Tambua kuwa kampuni au taasisi hiyo unayoiona haina maana leo, ndiyo iliyochangia kukufikisha hapo. Changamoto ulizokutana nazo katika kipindi chote cha ajira usiyoipenda, zilikuwa kichocheo cha kukuhamasisha kupambana kwa ari zaidi. Heshimu hilo.

Pia, pengine usingefanya kazi kwenye taasisi au kampuni hiyo usiyoipenda leo, mwajiri wako mpya asingekuona. Katika wasifu wako wa kazi ulimtaja mwajiri huyu usiyempenda leo. Uzoefu na ujuzi aliouvutiwa nao mwajiri mpya umeupata kwa kufanya kazi na mwajiri huyu unayeachana naye. Hilo angalau likusaidie kuwa mtulivu kwa maneno na vitendo. Kwamba hata kama ni kweli ulionewa, bado una sababu za kuthamini mchango wa mwajiri huyu.

Kwa upande mwingine, inawezekana umeachishwa kazi isivyo haki. Kutokuelewana na mkubwa wako kazini kumechangia kukuondoa. Katika mazingira haya, unaweza kuwa na ghadhabu. Una haki ya kukasirika. Lakini tambua kuwa ghadhabu ni dalili moja wapo ya kukuukana ukweli usioupenda. Kubali ukweli mchungu kuwa umefukuzwa kazi. Kisha fanya taratibu za kuondoka bila kuongeza maumivu yasiyo ya lazima.

Heshimu mkataba wa kazi

Kupata kazi bora zaidi ya hiyo uliyokuwa hakupaswi kukupa kiburi cha kuacha kazi bila kufuata taratibu. Kufukuzwa kazi, kwa upande mwingine, kunaweza kukuchanganya kiasi cha kukufanya uamue kuacha  kazi kinyume na mkataba wa kazi.  Usifanye hivyo. Rejea mkataba wako na mwajiri.

Mikataba mingi inamtaka mwajiriwa kutoa notisi ya kuacha kazi kwa muda wa kuanzia mwezi mmoja hadi miezi mitatu kabla ya tarehe ya mwisho ya kufanya kazi na mwajiri wako. Kimsingi, notisi ya kuacha kazi inalenga kumpa mwajiri muda wa kumtafuta mtu atakayechukua nafasi yako. Inakusaidia na wewe kukabidhi majukumu yako pamoja na vitendea kazi ulivyokabidhiwa.

Vile vile, inawezekana mwajiri wako wa sasa alikudhamini kupata mkopo katika taasisi za fedha. Pengine mlikuwa ya makubaliano ya muda maalum wa kufanya kazi kufidia gharama za masomo yako. Mtu mzima anayejitambua huheshimu makubaliano anayoyafanya na watu wenine. Usifanye kosa la kuondoka kazini kinyume na makubaliano uliyokuwa nayo na mwajiri wako.

Inaendelea

Maoni

  1. Good piece! Hongera mkuu

    JibuFuta
  2. Eglah hellen10/1/17 1:51 PM

    Asnte kwa makala kaka. Na hii imenisadia mm hasa maana nimeahachukua maamuz haya.

    JibuFuta
  3. Naomba mnisaidi nikipi mtu anatakiwa kufanya pale anapoamua kuacha kazi kwa sababu za kiafya

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Pay $900? I quit blogging

Heri ya mwezi mpya!