Nilichojifunza Katika Miaka 10 ya Kublogu

Kwa mara ya kwanza nililisikia neno blogu mwaka 2004. Wakati huo nilikuwa msomaji wa dhati wa safu ya ‘Gumzo la Wiki’ iliyokuwa ikiandikwa na Ndesanjo Macha katika gazeti la Mwananchi. Kwa kufuatilia anuani iliyokuwa ikihitimisha safu hiyo, niligundua kuwa sikuhitaji kusubiri  Jumapili kuweza kulisoma ‘Gumzo’. Anuani hiyo ilikuwa ni ya blogu ya kwanza ya Kiswahili ikiitwa Jikomboe.

Kwa karibu mwaka mzima nilibaki kuwa msomaji mwaminifu wa blogu hiyo nikifuatilia mijadala ya masuala yaliyokuwa yakinigusa sana. Jikomboe ilibeba maudhui ambayo siku kwa siku yalinipa changamoto nzito za kifikra. Hapa nazungumzia masuala ya kiutamaduni kama vile dini/imani, umuhimu wa lugha, historia na mambo kama hayo. 

Nilipobahatika kukutana na Ndesanjo Macha nchini Ufilipino. Mwingine ni Lova, mwanablogu kutoka Madagascar. Tulihudhuria mkutano wa uandishi wa Kiraia nchini Ufilipino. Picha: Jielewe
Blogu nyingine iliyokuwa na maudhui kama hayo na niliyoifuatilia kwa karibu sana iliitwa Harakati. Iliandikwa na Jeff Msangi ambaye hata hivyo baadae alianzisha blogu maarufu ya Bongo Celebrity. Jeff kama alivyokuwa Ndesanjo, naye alikuwa mwandishi wa safu ya kila Jumapili katika Gazeti la Tanzania Daima. Basi baada ya kusoma blogu kwa muda wa miezi kadhaa hatimaye mwezi Agosti 2005 nilianza kublogu

Nilianza kublogu bila kuwa na kompyuta wala mtandao wa intaneti. Nilitegemea huduma ya mikahawa ya mtandao wa intaneti katika taasisi za elimu nilimokuwemo au mitaani. Baadae nilibahatika kupata kompyuta mpakato. Hayo yalikuwa ni mafanikio makubwa kwa sababu ingawa sikuwa na mtandao wa intaneti angalau niliweza kuandika posti nikiwa chumbani na kisha kutumia muda mfupi kwenye mkahawa wa intaneti kuchapisha makala hiyo. Hatua kubwa. 

Kadhalika, nilianza kublogu bila kuwa na mwelekeo maalumu wa kimaudhui. Niliandika kihuria kama mwendelezo wa yale niliyoyasoma kwenye blogu nyingine, magazetini, vitabuni na hata niliyokumbana nayo katika mazungumzo vijiweni. Nilifanya blogu kuwa kitabu cha kumbukumbu ya mambo yanayonijia kichwani. Hata hivyo, kufuatia mijadala mikali iliyokuwa ikiendelea kwenye blogu za kipindi kile, nilianza kujikita kwenye masuala mahususi. Hivyo hatua kwa hatua masuala kama imani na mitazamo yalianza kuchukua nafasi yake kwenye blogu yangu. 

Kufikia mwaka 2008 tayari nilishaamua kublogu kuhusu masuala ya kijamii kwa maana ya kujaribu kutafuta majibu ya baadhi ya maswali niliyokuwa nikijiuliza. Nikaamua kuiita blogu yangu Jielewe. Lengo kuu lilikuwa kutengeneza kijiwe cha mijadala ya utambuzi. Ajabu, pamoja na kuwa na huduma ya mtandao wa intaneti niliyoikosa hapo awali, bado sikuweza kumudu kuandika mfululizo. Niliitelekeza blogu mara kwa mara. Harakati za kujipatia kipato zilizokwenda sambamba na uanafunzi unaodai gharama ya muda ilikuwa moja ya sababu.

Nilichojifunza

Yapo mambo mengi niliyojifunza kupitia blogu. La kwanza na kubwa, blogu imenisaidia kujieleza kwa uhuru. Blogu imenipa mamlaka kamili ya kuamua aina ya maudhui na mtindo wa kuyawasilisha maudhui hayo pasipokuingiliwa na wengine. Faida ya uhuru huu ni kunifanya nitafakari kipi nataka kukisema, kwa nani na kwa namna gani bila kulazimika kuongozwa na sera, itikadi au misimamo ya kitaasisi. Uhuru huu ni vigumu kuupata kwenye vyombo vingine vya habari vinavyoongozwa kitaasisi.

Pia, blogu zimenifunza umuhimu wa kutumia lugha ya Kiswahili katika kuwasiliana na ninaowalenga. Wakati naanza kublogu nilikitukuza mno Kiingereza. 'Bahati mbaya' sana wanablogu wenzangu hawakuonekana kukipa thamani yoyote Kiingereza. Nikajifunza jambo muhimu sana. Kwamba kama mwanablogu sina sababu yoyote ya kuendesha mijadala kwa lugha nisiyoitumia kijiweni na marafiki zangu. Niliishinda kasumba batili kwamba ili jambo liwe na maana lazima lijadiliwe kwa lugha ya kigeni.

Kadhalika, blogu zimenisaidia kujifunza kupitia kwa wasomaji. Blogu ni mijadala. Blogu ni mazungumzo. Katika mijadala ya blogu, nimeona namna watoa maoni walivyo na nafasi ya juu katika mjadala. Kwa hakika, wakati mwingine wasomaji huwa ni watu wenye maarifa zaidi ya mwandishi. Fikiria unapokuwa na wasomaji makini kama Profesa Mbele au Mubelwa na wengine wanaofanana na hao. Fikiria wanapoacha maoni kwenye maandishi yako. Unaweza kuona namna maoni yanayoachwa na wasomaji kwenye blogu, yanavyoweza kuchochea na kusisimua maarifa ambayo hayakutarajiwa. Hali hii ni tofauti na ilivyo kwenye vyombo vingine vya habari ambapo mwendesha kipindi, mwandishi au mmiliki hujivika jukumu la kumiliki maarifa anayoamini yanapaswa kupokelewa na wasomaji, wasikilizaji au watazamaji.

Jambo  na nne na muhimu ni uhuria wa maarifa. Kwamba kufahamu jambo fulani unalodhani ni muhimu hakukufanyi uwanyime wengine haki ya kulifahamu na kulisambaza kwa wengine kadri wanavyoweza. Ingawa ni kweli yapo mazingira ambayo haki fulani fulani za kiubunifu hulindwa kulingana na mtazamo na malengo ya mwanablogu, lakini kwa ujumla maarifa mengi kwenye ulimwengu wa kublogu ni huria. Ni kama hayana mwenyewe. Hili ni jambo muhimu.

Blogu pia zimeniwezesha kukutana na watu wengi kutoka kwenye maeneo ambayo kwa hali ya kawaida nisingekutana nao. Wengi wao wamekuwa marafiki zangu wa karibu mno kuliko hata watu ninaokutana nao kila siku. Nakumbuka niliwahi kusimulia namna nilivyotumiwa kitabu kutoka nchini Marekani na mwanablogu mwenzangu. Kitabu hicho nilikipata kwa gharama ya Tsh 0. Ndio kusema blogu zimenifungulia fursa nyingi zilizotokana na watu ambao hawakuwa katika mduara wangu wa marafiki. Blogu imenipa mtaji wa marafiki wenye maarifa.

Hata hivyo, najua enzi zinabadilika kwa kasi. Teknolojia mpya zinachukua nafasi. Kila siku zinatengenezwa zana nyingi za kiteknolojia zinazowezesha watu wa kawaida kujieleza kiwepesi. Teknolojia mpya zimewezesha uandishi kufanyika kwa kutumia sentensi fupi fupi. Na ndio maana pengine blogu nyingi zimetelekezwa.

Pamoja na yote hayo, bado ninauona umuhimu mkubwa wa blogu. Ni jukwaa la kutoa kile ninachofikiri kinaweza kuisaidia jamii. Ni zana ya kujadiliana na wenye maarifa kwa jina la wasomaji. Ninayo fursa ya kuifanya blogu kuwa uwanja huru wa masuala makini. Katika kufanya hayo, hata hivyo, naelewa changamoto zake. Penye changamoto, bila shaka, pana suluhu. Maana wahenga nao walisema penye nia pana njia. Kama nia ninayo, njia haitakosekana.

Maoni

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Haiba ni nini?

Ukuaji wa Kiakili na Kimwili kwa Mtoto wa Miaka 0 – 3

Uislamu ulianza lini?