Tumefinyangwa kuwa wakimbizi wa kudumu

KADIRI siku zinavyosonga mbele, ndivyo waswahili tunavyozidi kuwa watu tusiojitambua. Namaanisha kutokujifahamu sisi ni akina nani na tunatofautianaje na wasio watu wengine waliobaki katika uso wa dunia. Tunashindwa kuyaelewa mazingira yetu na thamani ya ustaarabu wetu ambao (huenda) ni ushenzi kwa wengine. Badala yake tunageuza ushenzi wao kuwa ndio ustaarabu rasmi wa jamii yetu. Tunashindwa kujua mwelekeo wetu kama watu wenye ustaarabu wao ambao ndio unaoleta maana ya maisha yenye alama ya Utanzania.

Matokeo ya haya matatu ni kurudi nyuma katikati ya hayo yanayoonekana kuwa ni maendeleo. Hapo ndipo tunapogeuka kuwa mazuzu wenye vitu ambavyo babu zetu hawakuwavyo lakini bado tukiishi hovyo kuliko hata walivyoishi wao. Kwa maana nyingine, tunakuwa watu wenye “zaidi” kwa habari ya vitu, lakini wenye “ukosefu” kwa habari ya thamani ya kweli ya utu wetu.

Swali tunalojiuliza hapa ni iwapo ni busara kung’ang’ania kuyatafuta maendeleo (kwa maana ya vitu na huduma) pasipo kwanza kuubaini ustaarabu wetu na kuchukua hatua za kujitambua kama jamii.

Je, ni busara kuwekeza katika elimu ambayo haitusaidii kujitambua sisi kama waswahili? Hebu nilisogeze swali pembezoni kabisa mwa upuuzi: Je, wananchi kuelimika katika mfumo ulioasisiwa na wageni kwa malengo ya wageni na kwa faida ya wageni ambao unaenda kombo na ustaarabu wa wananchi hao, huo nao ni werevu?

Maana tumekwisha kuona kuwa kadri raia (wetu) wanavyosoma na “kuelimika”, ndivyo wanavyozidi kuwa majuha. Hawaoni tena maana ya maisha ya kijijini. Hawaoni tena thamani ya ushirikiano wa kijamii. Hisia za ubinafsi na “kutafuta hela” zinatawala mioyo yao kuliko ustaarabu wa jamii walimotoka. Haya yote, yanawaweka mbali na jamii yao kiasi kwamba ni kujidanganya kufikiri kwamba watu wa aina hii wanaweza kuleta mabadiliko yoyote ya maana kwenye jamii yao. Hakuna mabadiliko wanayoweza kuiletea jamii yao maana hatma ya yote huishia kukimbia kimbia. Toka ofisi moja hadi nyingine. Fani moja kwenda nyingine. Na mwishowe ughaibuni kuyasaka maslahi binafsi.

Kumbe basi, katika aina hii ya elimu (isiyozingatia ustraabu na utu wetu) ni kazi bure kuwategemea “nshomile” (yaani hawa wanajiita wasomi) kuleta nafuu yoyote katika jamii. Ndio maana si ajabu “nshomile” hawa ndio walioweka mkono kuiuza nchi yetu kwa walanguzi wa kigeni. Ndio maana “nshomile” hawa ndio wahusika wakuu katika ujambazi wa rasilimali za nchi. Ndio maana “nshomile” hawa hawatulii kwenye fani zao. Sababu kwao, tafsiri ya mafanikio imegeuzwa. Kwao, kufanikiwa ni kuwa na ukwasi uliopindikia, kitu ambacho hakiwezi kuwa sehemu ya utu wetu. Kwao, kufanikiwa ni kujiletea “maendeleo” wao na wa kwao na wanaowajua.

Ndio maana nasema katika mazingira haya, ni busara kuanza upya katika ujenzi wa fikra sahihi za ustaarabu wetu ndani ya mioyo ya wanetu. Na hilo linaanzia katika elimu.

Elimu hii itokane na jamii yetu. Maana yake ni kwamba kwanza itusaidie kujielewa sisi na matatizo yetu. Sisi kwa maana ya utamaduni wetu, ustaarabu wetu na mweleko wetu. Matatizo yetu kwa maana ya changamoto zinazotukabili sisi kama watu wanaojielewa katika kutafuta namna ya kusonga mbele.

Elimu hiyo haiwezi kuwa “hii” ambayo mbali na kutufunza yasiyohusiana na sisi, imefinyangwa kwa mfumo unatuweka mbali na yale yanayohusiana na sisi. Ndio maana sishangai –katika mazingira ya elimu zuzu kama yetu– nshomile hawataki kuachana na matumizi ya kiingereza katika mfumo wa elimu. Maana inahitaji muujiza wa pekee kwa mtu aliye zao la utumwa, kuubaini utumwa. Na akifanikiwa kubaini hawezi kujinasua, maana kishakuwa mkimbizi. Mkimbizi wa utu wake. Mkimbizi wa ustraabu wake. Mkimbizi wa utamaduni wake. Mkimbizi wa kila kitu kinachohusiana na jamii ya watu wake.

Sasa kwako ndugu msomaji: Je, ni namna gani umefinywangwa kuwa mtumwa asiyejitambua na wa kudumu? Jielewe...

Maoni

  1. Topiki ngumu hii.:-(

    Nikikunukuu``
    Tunashindwa kujua mwelekeo wetu kama watu wenye ustaarabu wao ambao ndio unaoleta maana ya maisha yenye alama ya Utanzania. ´´-mwisho wa nukuuu.

    Hapa tatizo lijitokezalo ni ; Kwanza Utanzania ni nini hasa ukizingatia Tofauti za waitwao Watanzania kutoka kwa Mtanzania mmoja mpaka mwingine na kutoka Jamii moja iliyopo Tanzania mpaka nyingine?

    Nukuu``
    Elimu hii itokane na jamii yetu. Maana yake ni kwamba kwanza itusaidie kujielewa sisi na matatizo yetu. Sisi kwa maana ya utamaduni wetu, ustaarabu wetu na mweleko wetu.´´- mwisho wa nukuu.

    Hivi nni kweli Tanzania ina jamii moja yenye matatizo yanayofanana, tamaduni zinazofanana na tafsiri ya ustaarabu inayofanana kitu kiwezacho kufanya mwelekeo wa wote uitwe wetu?

    Nukuuu``Elimu hiyo haiwezi kuwa “hii” ambayo mbali na kutufunza yasiyohusiana na sisi, imefinyangwa kwa mfumo unatuweka mbali na yale yanayohusiana na sisi.´´- mwisho wa nukuu.

    Je sisi ni kina nani? Je mafisadi na waaminio kuelimika ni kubonga ung'eng'e sio akina sisi pia ambao elimu iliyopo inasaidia kwa hilo?

    Je, ni namna gani umefinywangwa kuwa mtumwa asiyejitambua na wa kudumu?

    Hivi hakuna uwezekano kuwa kila Binadamu amefinyangwa kuwa mtumwa asiyejitambua na wa kudumu hasa ukizingatia hakuna Binadamu afaye akijua yote na labda kwa kila Binadamu kila siku ya maisha yake ni shule atake asitake?

    NAENDELEA KUWAZA na asante kwa kuchokoza fikira Mkuu!

    JibuFuta
  2. Wakati wewe unatafakari haya wenzakoo wanatengeneza mitaala inayoendana na wenzetu wakiita ya `kimatifa' manake nini, tuendane na wenzetu kifikira, wakati hata kutenegeneza pini tunahitaji watu toka nje.
    Elimu yetu inazidi kuwa ngumu kwasababu ili tufanye kitu fulani tunahitaji kutafuta kutoka kwa wenzetu, na kama hawo ndio tunaona wameelimika basi hata kile wanachokifanya wale wao wanaowaita `watukutu' kwetu ni jambo la `kisasa' kwa maana kuwa tunaenda na `wakati'

    JibuFuta
  3. Sikumshangaa mtu yule aliye sema ya kuwa anaombea viongozi wa wakati huo waliokuwa madarakanai wayeyuke na kuwa kama moshi ili tuanze na viongozi wapya wenye fikra zinazoendana na wakati!

    JibuFuta
  4. Wakati mwingine nakubaliana na wewe Chib..inauma sana..ni kama vile kuna watu wamezaliwa kuwa viongozi!

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Pay $900? I quit blogging

Heri ya mwezi mpya!