Blogu bora kwa mwaka 2009!

Mwaka jana umepita kwa namna yake. Namshukuru Mwenyezi Mungu amenifikisha mwaka huu salama. Japo sikuwa hewani mwishoni mwa mwaka, lakini nimekuwa nikitafakari kidogo namna mwaka ule ulivyoenda katika maeneo kadhaa ya maisha yangu. Mafanikio kwa Matatizo. Furaha kwa huzuni. Kupanda na Kushuka. Kupiga hatua mbele katika eneo moja na kurudi nyuma kwingineko. Yote yamekuwa sehemu yangu kwa mwaka uliopita.

Nimekuwa msomaji wa blogu karibu zote zilizo hai. Na kwa kweli nimejifunza maarifa mengi makubwa bila kuyagharimia. Waandishi wake waliyagawa bure na uone ilivyo ajabu, maana waliweza kujibizana na wasomaji wao kwa lengo la kupanua mjadala.
Na ni hakika kwamba hivi sasa blogu zimeanza kuchukua nafasi ya magazeti na televisheni, au angalau kupambana na vyombo hivyo vikongwe. Umaarufu wa magazeti ya kununua taratibu unaanza kupotea.

Katika blogu za Kiswahili jambo la tofauti hivi sasa ni maudhui aina aina yanayoandikwa. Nakumbuka miaka mitatu au minne iliyopita, karibu kila blogu ilikuwa ni ya uchambuzi wa kisiasa. Tuliiga magazeti ya kale kwa kujaribu mara zote kujadili matukio na wanasiasa. Lakini hivi sasa tuna karibu kila aina ya maudhui (ya kina). Hiyo ni kuanzia siasa, mashairi, dini, mitindo, upishi, falsafa, jamii, mahusiano, elimu-nafsi nk.

Kibinafsi kabisa ningependa niwashukuru wanablogu wote kama jamii kwa namna walivyo na moyo wa kuwashirikisha wengine kile wanachokifahamu. Nimejifunza mengi mwaka huu uliopita.

Ninajua namna ninavyoelimika kutoka watu wa tabaka tofauti tofauti.
Hata hivyo, hata ni ka mtindo changu tu cha mwaka huu kasikusumbue. Kwamba nimeona ni vyema niwapongeze wanablogu watatu ambao wamenipa changamoto kubwa sana ya kifikra kwa mwaka 2009. Wanablogu hawa karibu kila siku wameniacha na hoja nzito sana za kutafakari hata niwapo nje ya mtandao. Wamenisababisha niendeleze mijadala na marafiki zangu ambao najua hawasomi blogu. Naomba kuwatambua kiujumla jumla bila kuorodhozesha sababu zangu:

1. Chakula kitamu inayoendeshwa na Mwalimu Masangu Matondo.
2. Kulikoni Ughaibuni inayoendeshwa na Evarist Chahali.
3. Changamoto yetu ya Mubelwa T. Bandio

Natumaini kuwa wanablogu hawa wa mwaka kwangu, wataendelea kufanyika sehemu ya ratiba yangu ya siku kwa mwaka unaoanza.

Hizi ni tatu tu, lakini ukweli ni kwamba nasoma blogu zote na siwezi kuziorodhesha zote hapa.

Mabarikiwe nyote!

Maoni

  1. Mimi bila kusita BWAYA , ni kwa miaka kadhaa sasa BLOGU yako kwangu ni bonge la changamoto na ni lazima nipite kuchungulia unafikiria nini.

    JibuFuta
  2. Asante Simon kwa ushirikiano. Najua tumekuwa karibu sana kwa kipindi kirefu sana. Na niliyoyapata kwako unayatambua.

    Najivunia kukufahamu, najivunia ukaribu tulionao. Amani kwako Simon!

    JibuFuta
  3. Duh!!
    Hii sikuitegemea kwa kuwa haikuwa chanzo cha kuandika. Sikuwaza kuwa kuna wanaopata changamoto mbalimbali kutoka kwenye BLOGU YETU maana pale najifunza zaidi ya ninavyofunza (kama ambavyo niliandika hapa http://changamotoyetu.blogspot.com/2009/12/blogu-ni-shule-wajifunzao-ndio-wafunzao.html)na maoni yenu wapendwa ndiyo yaletayo chachu na changamoto za kuandika mengine mengi zaidi. Hapa kijiweni ndipo nilipopata mawazo mengi ya kuanzisha blogu kwa namna muionavyo. Niliwaza saaana nini la kufanya baada ya kupata ushawishi wa kuanzisha blogu na kwa kutembelea kjijiwe hiki, cha Kamala, kwa Mkodo na watambuzi na wachambuzi wengi nikaona ni vema kuandika kwa suluhisho kuliko matukio kama picha.
    Na sasa niomepata changamoto toka kwa Dada Mija kuwa tuangalie mambo kwa JICHO LA NDANI ambayo inaendana na ile aliyoitoa Master T alipojibu salamu za mwaka kuwa tuelekeze maandishi kwenye kuchochea suluhisho kuliko matatizo.
    Naamini mwaka huu kutakuwa na mafanikio na wenzangu na mimi wanaochipukia wataleta changamoto kubwa kufanikisha hili. Kwani ninyi mlianza kuonesha njia nasi twafuata
    SHUKRANI NA TUKO PAMOJA

    JibuFuta
  4. Kaka Bwaya,mimi napenda tutilie msisitizo kuhusu JUMUWATA.

    kATIKA jicho la Ndani nitasisitiza sana kuhusu jumuwata.

    haiwezekani miaka yote tumekaa na kuangalia jumuwata ikijifukia yenyewa au kufukiwa.

    2010 katika jicho la ndani ni kufufuwa jumuwata.

    JibuFuta
  5. Bwana Bwaya;
    Hata mimi hili sikulitegemea na pengine Mzee wa Changamoto ameshanisemea pia. Naamini kwamba nimeshabadilika tangu kuanza kublogu. Kuna mambo mengi sana ya kujifunza hata kama uwe "umesoma" namna gani. Japo muda wa kukaa na kuandika kikamilifu haupo, huwa naandika kwa kuparura parura tu na sikuwahi kufikiri kwamba ninayoyaandika hapa yanavutia na kufikirisha. Na kutokana na ukosefu wa muda kuna wakati huwa nakosa muda wa kutoa maoni ya kina katika blogu mbalimbali mojawapo ikiwa hii. Kwa mfano ningali bado naandika maoni kuhusu ule mjadala uliozushwa na mchangiaji makini GODWIN HABIB MEGHJI kuhusu uhusiano wa lugha na kufikiri.

    Asante Bwana Bwaya na tuendeleeni kubadilishana mawazo, kuimarishana kifikra na kuipigania jamii. Natumaini kwamba mwaka huu mpya utakuwa mwema zaidi!

    JibuFuta
  6. Wanasema ukweli huwa unajitenga. Maoni ya Bwaya ndio ukweli na mtazamo wa wasomaji wa blogu wa mara kwa mara.

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Uislamu ulianza lini?