Watu wanapata taswira gani wanapokutazama?

Binadamu anao uwezo wa kujenga taswira yake - namna anavyoonekana - kwa wengine kwa kadiri apendavyo awe. Binadamu anaweza kuamua kuonekana mtu wa heshima zake, ama hata kuonekana mtu asiye na heshima zake. Uamuzi wa kujenga taswira hiyo, self-image kwa msisitizo, uko mikononi mwake yeye mwenyewe.

Kwamba tunafikiri wengine wanatuchukuliaje ni suala la kujenga taswira zetu. Kwamba zaidi ya kule kujitathimini wenyewe, kujiangalia kwa macho yetu wenyewe, tunajaribu kujitazama kwa macho ya watu wengine. Tunajaribu kujifikiria kwa miwani ya wanaotuzunguka. Tukijiuliza swali kubwa: hivi huyu jamaa ananionaje hapo alipo? Self-image. Si tu kujiaminisha kuwa tu watu wa aina fulani kwa kutumia vigezo vyetu, bali kujaribu kurudusu, wengine wanatuonaje.

Hatuwezi kujifahamu sisi ni akina nani kwa kujiangalia kwa macho yetu wenyewe. Macho yetu hutudanganya na mara zote hutafuta kutupendelea. Macho yetu hutafuta kutufanya tujisikie vizuri kuhusu nafsi zetu. Hivyo, tunapotaka kujifahamu kwa usahihi, tunashauriwa kujitazama kwa macho ya watu wengine. Na kwa kadiri tunavyochangamana na watu wa aina mbalimbali, ndivyo tunavyojigundua sisi tu watu wa aina gani. Mtu anayejifungia mwenyewe, akifanya kila kila kipekeyake, inaaminika kuwa hawezi kujifahamu sawia.

Ili kuifahamu taswira yako, unajivika viatu vya anayekuangalia, unakuwa yeye haswa, halafu unajigeukia na kujaribu kujitazama ( kama vile unamwangalia mtu mwingine), ukijaribu kutathimini anavyokuona.

Taswira hiyo unayoipata, kwa macho ya mwingine, ndicho hicho tunachokiita self-image. Taswira amabyo huweza hubadilika kulingana na mtu anayekuangalia. Na mara nyingi, binadamu hujaribu kujenga taswira tofauti tofauti kulingana na hadhi ya huyo anayekuwa naye.

Kwa mfano, unapokuwa na mtu unayemheshimu, unaona ya kwamba utataka akuone katika namna fulani iliyo tofauti sana na ile ambayo utakuwa nayo uwapo na mtu usiyemthamini. Vijana hubadili self-image zao kwa wachumba ama rafiki zao. Wanafunzi kwa walimu wao. Waumini kwa viongozi wao wa dini. Watoto kwa wazazi wao. Wafanyakazi kwa makuu wao. Hiyo ni kuonyesha kuwa self-image zetu hubadilika badilika kulingana na mlengwa.

Hutokea yakafanyika makosa ukajikuta ukiwa na sura fulani kwa mtu asiyekusudiwa. Kwa mfano umefanya kituko ambacho, pamoja na kutokuwa kibaya, hakikupaswa kufanywa kwa mkubwa wako wa kazi ila kwa rafiki yako. Hapo unakuwa umeharibu sura yako, ama defacing kwa msisitizo.

Inapotokea imekuwa hivyo, huwa kuna juhudi za dharura ambazo huchukuliwa kutengeneza upya self-image yako. Watu wengine wanaita kujibaraguza. Kufanya fanya mambo fulani ili kuharibu uharibifu uliotokea kwa lengo la kuhakikisha kuwa ile sura ya mwanzo inabaki kuwa ilivyo.

lakini wapo watu wanaoamini kuwa tunapaswa kuwa na sura moja kwa watu wote. Kwao kujenga taswira inayobadilika badilika ni udhaifu. Kwamba sura unayokuwa nayo kwa watu fulani, uiendeleze hiyo hiyo kwa watu wa aina zote. Wewe una maoni gani?

Siku njema.

Maoni

  1. Mkuu,
    umenikumbusha mbali sana,wakati nikiwa na nywele za msoko wengi walikimbia na kusema mvuta bangi,baada ya kukata nywele za msokoto wakasema nimeokoka na hii yote inatokana na taswira za watu.Kwasabau unapenda kusikiliza reggae na documentaries za reggae basi wanakimbilia na kujaza wanayo jua.Topic imetulia sana.

    RASTA HAPA.

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Tabia za Mtoto wa Miaka 0 – 3 Kimahusiano na Kihisia

Pay $900? I quit blogging