Hivi ni laana ama ni mdudu gani?

Niliwahi kumsikia "mwinjilisti" mmoja aliyekuwa akichapa injili mitaa ya Kariakoo. Siku hizi ni jambo la kawaida kukuta watumishi hawa wanaoitwa wa Mungu wakifanya "vitu vyao" hadharani bila kujali haki za wengine. Kelele nyiiiingi kisa wanasema habari za Mungu. Kwa hiyo kimsingi haikunishangaza.

Huyu bwana alikuwa "siriaz" kweli na kazi yake kiasi kwamba ungemhurumia kumwona akisema na watu wasiomsikiliza wala kujali anachosema. Jua lilikuwa kali na alikuwa kavaa koti zito. Joto la Dasalama tunalijua. Japo sikumsikiliza, nilihisi kazi yake ilikuwa ni "kuwarejesha kondoo katika zizi la Bwana".

"Afrika na watu wake, imelaaniwa!" alipayuka huyu bwana huku akitembea kwa madaha. Akageuka huku na kule, akanyanyua biblia yake kuuuuubwa akaendelea: "Enyi uzao wa Hamu, mmelaaniwa na laana yenu inakaa!".

Kwangu mimi maneno haya yalininyong'onyeza mithili ya mtu aliyenyeshewa mvua. "Hivi anajivunia nini kusema maneno haya? Hata kama ndivyo anavyoamini, hivi maneno haya yanamsaidia vipi kuwarejeza kondoo anaowapayukia juani?". Nilijisemea moyoni. Hata hivyo, niliondoka tu kwa shinikizo la niliyekuwa naye.

Hiyo ilikuwa changamoto kwangu, maana ilibidi kuirejea biblia kusoma "upuuzi" wa huyu bwana. Na kwa kweli katika Kitabu cha mwanzo 9:24-27 nilikutana na maneno hayo. Kisa kinaelezwa kwamba wakati Nuhu amelewa, mwanaye mmoja aitwaye Hamu alimwona akiwa uchi, akawaambia nduguze. Ikawa hao ndugu zake waliposikia hayo wakaenda kinyume nyume wakaufunika uchi wa baba yao, hawakuuona. Biblia inaandika kwamba Nuhu alipozinduka na kusikia kuwa Hamu "alimchungulia" akamwaga radhi. Hamu akawa amelaaniwa.

Kifungu hiki katika biblia kilinichanganya na kuna mambo kadhaa yalinishangaza. Kwanza, iweje Nuhu amlaaani mtu ambaye (naamini) aliuona uchi wake kwa bahati mbaya? Maana akili yangu inanituma kuwa Hamu ndiye alikuwa wa kubariki. Maana alipouona uchi wa babaye kwa bahati mbaya alichukua hatua ya kuwaambia nduguze ambao ndio walimfunika. Kosa la Hamu ni nini? Iweje alaaniwe kwa sababu ya bahati mbaya?

Lakini vilevile nashindwa kuelewa iweje Hamu ndiye awe Mwafrika? Imeandikwa wapi mbona katika biblia sioni popote panapothibitisha hilo? Hapo sijajua sana.

Hata hivyo katika kutafakari, kuna mambo ambayo pia yanaweza kuwa ni uthibitisho wa madai haya. Hivi kwa nini waafrika tuko nyuma namna hii? Naambiwa na waliosoma historia kwamba tuliwahi kuwa katika fungu moja na watu weupe (Sitaki kuwaita wazungu maana ni kuwatukuza wawe sawa na Mungu). Kwa nini wametuzidi? Zinatolewa sababu nyingi. Oooo, mapinduzi ya viwanda sijui teknolojia sijui nini...waaaapi bwana, tulishindwa nini na sisi kuwa na yayo hayo?

Tunaambiwa tuliuzwa kama bidhaa. Yaani mtu anakuja anawachukua mpaka Bagamoyo wala hamjiulizi! Mnafika pale mnapigwa bei, kwenu sawa tu! Hivi kama sio laan ni nini?

Simulizi la akina Mangungo wa Msovero ndio buuure kabisa. Unanyeshwa pombe unapokea vijizawadi halafu unatia saini mkataba amabao hata hivyo huulewi! Akili ya wapi hii...mnake kuja kustukia kumbe nchi umeiuza! Kama sio laana ya Nuhu ni nini hii?

Unajua bwna amabo mengine tufikirie. Hivi wewe anakuja mzungu anachimba madini anabebea kila kitu mapaka na mchanga halafu wewe anakuambia atakuachia mrahaba wa asilimia tatu, wala hustuki. Unatia saini! Hivi ni kweli?

Unafuta masomo ya Historia, Uraia na Jiografia kwa wanafunzi wako kisa tu ndio masharti ya mkubwa. Matokeo yake unabaki kuwafundisha watoto mambo ya utandawazi, unayapa kisogo mambo yanayowajengea uzalendo. Na wala sio kwamba huelewi, unajua. Jamani hii nayo siyo laana kweli?

Kuna maeneo mengi ambayo mimi nafikiri kuna hitilafu ambayo si ya kawaida. Nilikuwa nafikiri tabia yetu waafrika ya kuwapapatikia hawa jamaa weupe. Yaani mambo mengine yanachekesha kweli. Waafrika wenzako huwa huna "taim" nao leo kaja "mzungu" unajidai ndio makarimu kuliko wote. Unamtetemeka nini? Au ndio ile laana ya Nuhu kwamb utakuwa mtumwa wa wenzako?

Ndesanjo anapiga kelele sana kuhusu kuitunza historia yetu. Watu tunang'ang'ania mambo ya kizungu zungu...uzungu zungu mwingi kumbe tunatumikia laana ya Nuhu. Eti eeeh? Unabisha? Kiingereza cha nini mashuleni wakati wanaofundishwa hawakielewi? Ukiwauliza mtabishana mpaka kesho. Kumbe watu wanadhani kujua kiingereza ndio kusoma. Hii inaweza kuwa laana! Kabisaaa! Kwamba tuwatumikie hawa jamaa.

Kwa hiyo nasema biblia kusema kweli inachanganya. Mimi hapo sijaelewa. Na anajua nikimwuuliza Mchungaji ntaonekana natimizqa dalili za mwisho wa dunia. Kwamba watu watajifanya kuwa wanajua sana. Naomba kuhitimisha hapa.

Maoni

  1. hadithi ya Hamu ilitumiwa sana na makaburu, ilitumiwa na mabwana wa watumwa marekani nk.

    ukiamini una laana basi umekwisha!
    Kwani si ni katika Biblia hiyo hiyo ambapo Yesu alikuwa akifukuza magonjwa, ibilisi na laana zote?

    JibuFuta
  2. Huku kuwa nyuma kwa Wafrika, niliwahi kusoma kwamba kumechangiwa kwa kiasi kikubwa na hali ya kijiografia ya Afrika, kwa maana kwamba Muumba aliifanya Afrika isiwe na matatizo ya kijiografia kama baridi kali,majanga ya asili kama mafuriko, vimbunga, matetemeko ya ardhi n.k. Ndio maana hatukuhitaji kujibidiisha kwa lolote kwani maisha yaliweza kwenda bila shida. Ukisikia njaa unaokota matunda mwituni au unawinda wanyama ambao ni wengi, jua likiwa kali sana unakaa chini ya mti, mvua ikinyesha unajificha pangoni. Alimradi maisha yasiyokuwa na taabu. Ikumbukwe kwamba magonjwa kama malaria hayakuwepo wakati huo.
    Je ni kweli kwmba hali hii ndio iliyofanya wenzetu weupe wapate maendeleo makubwa kuliko sisi weusi?

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Uislamu ulianza lini?