Sauti ya Umma inapomtaka Baraba...

Najua wengi hawasadiki mafundisho ya kitabu kiitwacho biblia. Mniwie radhi, nikirejee kidogo.
Katika kitabu cha Mathayo 27:15-26 kuna tukio ambalo linasadifu suala la demokrasia ya enzi hizi. Hapa kuna fundisho la jinsi ambavyo demokrasia ya watu inaweza kuchezewa kama wapendavyo waungwana wachache wenye nafasi ya kufanya hivyo.
Katika Uyahudi hiyo, wakati wa Pasaka, Pontio Pilato, Mkuu wa Dola ya Rumi katika Uyahudi , alikuwa na utaratibu wa kumfungua mfungwa mmoja wakati wa Pasaka (Mat. 27:15). Lakini Pilato ili kufanya hivyo inasemekana ilimpasa kupata ridha ya wananchi wa Uyahudi ile, ili amweke huru mmoja wa wafungwa kwa mujibu wa katiba yao.
Basi, ilitokea katika Pasaka mmoja Yesu Mnazareti akawa amekamatwa kwa kosa la kuwakosoa watawala kwa kutangaza mambo ambayo hayakupendeza machoni pao. Nafikiri Yesu alikuwa tishio kwa watawala hao.
Kukamatwa kwa Yesu kulikuja baada ya Yuda Iskariote kugawiwa takrima ya nguvu (Ni kama fulana siku za leo) iliyomshawishi kusahau mafundisho yote ya Yesu na badala yake, akamsaliti. Hivyo Yesu akatiwa mikononi mwao, ahukumiwe kifo.
Biblia inasema Pilato alipokuwa akipanga kumwangamiza Bwana Yesu, alionywa katika ndoto kuwa asithubutu kumwua mtu huyo ambaye kimsingi hakuwa na hatia. Pamoja na Yesu, alikuwapo mfungwa mwingine mashuhuru (ukipenda, sugu) aitwaye Baraba, mfungwa aliyekuwa amefungwa kwa ukatili aliokuwa akiwafanyia wananchi.Rejeo ni Luka 23:19. Bwana huyu alikuwa mnyang’anyi, na mfitini, ambaye kwa nujibu wa sheria za Uyahudi alistahili kusulubiwa msalabani wakati huo wa Pasaka. Baraba alikuwa raia katili haswa.
Pamoja na kwamba Pilato na wananchi wengine waliujua ukweli baina ya watu hao waliotofautiana mno kimaadili, ilibidi kwa mujibu wa katiba, awalete wote mbele ya Wayahudi asikie wanasemaje. Kwa maana nyingine, Pilato alitaka sauti ya wengi iamue hatima ya watu hawa.
Kitu cha ajabu, Wakuu na Wazee, watu waliokuwa na nyazifa nzito katika serikali walipita pita huku na huko kuwashawishi kwa ghiliba Wayahudi kumtaka Baraba badala ya Yesu asiyena hatia(Soma Mat. 27:20, Marko 15: 11) Basi Wananchi wakashawishika kumtoa kafara Yesu Mnazareti. Hapa ni lazima tukubaliane kuwa wapo watawala wengi ambao wapo kwa maslahi yao ingawa wanawatumia wananchi kufikkia malengo yao.
Wakati wa kupata ridhaa ulipofika, Pilato akawauliza “Niwatolee nani kati ya Yesu na Baraba?” Kwa mshangao wake, kura zote zikawa kwa Baraba, fisadi na mzandiki. Wakasema “Tupe Baraba..msulubishe Yesu!” Kwa maana nyingine sauti zao zikashinda ki Tsunami (Luka 23:23).
Hapa ndipo ninaposhangaa sauti ya wengi kumtetea mwovu fisadi, mla rushwa mtu ambaye asingefaa kwa lolote alhali wakipitisha hukumu ya kifo kwa mtu asiye na hatia!
Huo ndio ukawa mwanzo wa safari ya Yesu Mnazareti kuelekea Golgotha alikosulubiwa kwa ridhaa ya wengi, huku Pilato mwenyewe akinawa mikono yake kuwa sauti hiyo ya kishindo ilikuwa na walakini.
Ninajiuliza jambo moja. Hivi hawa Wayahadi hawakujua hasara ambayo wangeipata kwa kushinikiza Mnyang’anyi Baraza aachwe huru? Hivi hawakujua kuwa walikuwa wanakaribisha balaa katika jamii yao tena?
Ni wazi, kwa mukhtadha huu, kuwa sauti ya watu si lazima iamue ukweli. Kila jamii hufanya maamuzi kwa sababu fulani fulani ambazo hata hivyo si lazima ziwe takatifu na za manuafaa.
Tuliwahi kufanya uchaguzi katika darasa letu mwaka jana kumchagua Kiongozi wa darasa. Walijitokeza wahanga wawili wakitaka tuwachague. Mmoja alikuwa mtu wa hivi hivi tu, mtu asiye na utaratibu. Kwa lugha ya moja kwa moja, mhuni. Mwingine, wote tulimjua kama mtu makini kwa maana ya umakini.
Niliamini kabisa kuwa darasa zima lingemchagua huyu wa pili atusaidie, lakini masikini sivyo ilivyokuwa. Leo tuna Kiongozi wa Darasa ambaye ni kituko na kwake yote ni “Fanyeni mtakavyo!” Sijui kwa nini bwana huyu alikubalika hivyo.
Watu wengi wakisema na iwe hivi usidhani mara zote kuwa wana busara sana. Wanaweza kuwa wanafanya hivyo kwa ujinga (kutokujua) au kwa sababu pamoja na kwamba hawanufaiki kwa lolote na maamuzi wanayoyafanya bado wamejikuta wakifanya wanavyofanya.
Katika uchaguzi, kwa mfano hii laweza kudhihirika. Kama jamii yenyewe imeota mizizi katika ufisadi na ula rushwa, hatuwezi kutarajia kuwa watamtaka “Yesu Mnazareti” ambaye atatofautiana nao sana! Kwa watu hawa “Baraba” lazima awe ni chaguo lao kwa kishindo. Ndivyo ilivyo.

Maoni

  1. Kazi nzuri sana hii ya uhusiano uliopo katika dini hapo zamani na jinsi ambavyo tunasukuma gurudumu letu siku hizi.Unajua kuna hili neno "demokrasia" .Hili nadhani linatupeleka shimoni kila siku kama sio kutafsiriwa vibaya.Wananchi wanapomchagua kiongozi kutokana na rushwa hiyo ni demokrasia gani?

    JibuFuta
  2. Dear Chris,

    nilishangaa kuna kipindi nilisikia Austria walitafuta mgombea uraisi wakamkosa kwa kuwa watu hawakujitokeza! mjadala huu wa sasa unaongelea demokrasia! yes matumizi ya demokrasia ni mazuri zaidi au ni sahihi kama wale wananchi wanajua hatima ya kila uamuzi wanaoufanya! ni muhimu jamii ikapigwa shule! ninaogopa sana sasa hivi naona kabisa kuwa huko bungenii itakuwa ni kiwanda cha umeme maana watu watashusha neti!

    JibuFuta
  3. Ni kweli bwana Jeff, kama unavyosema. Demokrasia katika nchi zetu hizi, inachezewa na wachache wenye mamlaka. Wanatutumia sisi kwa manufaa yao.
    Mwaka huu walikuwa na sisi mitaani, utafikiri wanatupenda, lakini wapi bwana? Wamepata walichotaka tutawaona baada ya miaka mitano. Ama ndani ya mashangingi yao barabarani kama tutafanikiwa kwenda Darisalama.
    Ndio mambo yalivyo?

    JibuFuta
  4. Inavyoonekana ni kwamba wananchi wametumia Demokrasia yao kulifanya Bunge liwe la cahma kimoja. Sasa hii ni nini kama sio moja ya kamati katika cham...sio bunge tena!

    JibuFuta
  5. Kweli kabisa kuwa sauti ya wengi inaweza kuwa isiwe sauti ya haki au kweli. Au yenye manufaa. Ingawa mtazamo wangu kwa kitabu ulichotumia katika mfano wako sio sawa na mtazamo wa Wakristo au hata Waislamu, nimependa mfano ulioutoa.

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Uislamu ulianza lini?