Bongo flava imevamiwa na wababaishaji

Siku hizi raia wanapambana na ufukara wao kwa mbinu nyingi.Zipo zilizo halali na hali kadhalika zipo zilizo haramu. Ndio maana utaona kuwa tatizo la ujambazi limekuwa likinona na kunenepa kila uchao.
Watu wanatumia nguvu kunyanganya mali za wengine, mchana kweupe. Watu wanavunja nyumba za watu, wanachukua (iba) kila kilichomo mumo. Usije ukadhani kuwa wanapenda, ni mfumo unawalazimisha kutenda matendo hayo bila hiari. Ashakumu si matusi, afadhani ujambazi huu kuliko "ule mwingine" unaofanywa na wachache wanaodhani wana meno kuliko sisi kwa kutumia ile iitwayo demokrasia.
Katika kukabiliana na ukata wa maisha, siku hizi kumeibuka kundi la vijana wengi wakilazimika kujiunga na miradi ya shughuli za usanii wa aina kadha wa kadha. Muziki mpya, maarufu kama Bongo flava, ukiwa ni moja wapo. Ni mradi usiodai gharama kubwa kama vile elimu ambayo siku hizi haipatikani kiurahisi.
Kimsingi, hii ni njia halali ambayo faida zake si haba. Kwanza, ingawa haijawa ajira iliyorasmishwa, imekuwa unga "kidonyo" kwa vijana wachache wenye dhamira na hilo. Vilevile, ni muziki huu ndio uliofanikiwa kuziteka nyoyo za wananchi wengi wa kawaida, wapenzi wa muziki na midundo motomoto. Ni kwa sababu hiyo, Bongo flava imesaidia kueneza ujumbe wa kuwahamasisha wananchi kuhusu suala la kujiletea maendeleo yao wao wenyewe.
Sitaki kubeza kazi nzuri za baadhi ya wasanii, ambao ukisilikiza mistari yao, utagundua kuwa hawakukimbilia muziki kujiokoa na ukosefu wa ajira. Ni watu wenye vipaji. Nyimbo zao zimebeba dhana kamili iiyobebwa katika fani inayokidhi haja.
Nimewasikia wakituelisha kuhusu umuhimu wa kuwa makini wakati wa uchaguzi, kujua nafasi zetu wakati wa kura ili kuepuka tatizo la kuwaweka madarakani watu wezi na walanguzi wanaotumia migongo yetu kujilisha. Wapo wanaokemea tabia zisizopendeza, zanazofanya baadhi ya watanzania. Wengine wanasihi jamii kubadilika, ili kujiokoa na janga la UKIMWI, kazi ambayo ni nadra kufanywa kwa dhati na wanasiasa wetu. Huo ni upande wa kwanza wenye matumaini.
Hata hivyo katika upande wa pili, nasikitika kusema kuwa Bongo flava imevamiwa na wababaishaji wasiojua wajibu wao katika jamii. Wababishaji wanaopenda sifa za chee (cheap popularity, kwa msisitizo) kwa kuimba nyimbo za majigambo yasiyo na msingi kwa kigezo cha kuburudisha jamii.
Ni kweli kuwa pamoja na maudhui yake, fasihi vilevile inawajibika katika kuburudisha wanajamii, ambao kimsingi hukumbana na mengi ya kukatisha tamaa na kutupunguzia ari ya kufanya kazi maana hisia zetu zinakuwa zimejeruhiwa. Hapo liwazo ni muhimu.
Tunajua kuwa Tanzania ina matatizo mengi sana ambayo kama wasanii wangekuwa makini, wangeweza kufanya kazi ya kuonekana katika kuleta mabadiliko makubwa katika jamii yetu. Mchango ambao ungelitukuka ama kwa hakika. Lakini inavyoonekana Wasanii (na kweli ni wasanii/waigizaji) wamejikita zaidi katika kupigana vijembe wao kwa wao. Mtu anahisi kuwa fulani hampendi, basi anamtungia mistari. Huyo naye anakwazwa na mistari hiyo, anaingia studio kwa majibu. Basi alimradi ni biashara isiyo na mwenyewe. Haina kichwa wala miguu.
Mtu tunamjua ni masikini kama walivyo watanzania wengi, lakini unakuta katika video yake anaigiza maisha ya ufahari uliopindukia. Magari ya kifahari (ya kuazima), maisha ya ngono zembe na ulevi wa pombe uliokithiri. Mtu kama huyu bado eti anataka watanzania wajifunze kwake! Kama wapo wakujifunza kwake, basi ni wendawazimu.
Wanasahau kuwa midundo mizito yenye kusindikiza ujumbe wa mipasho kwa mahasimu wao haiwasaidii wasikilizaji. Wengine wamejikita katika kutuimbia mambo ya kimapenzi zaidi, wanasahau kuwa Mtanzania mwenye njaa, hawezi kula mapenzi. Mtanzania anayetishiwa na umasikini hawezi kusaidiwa na aina ya muziki tunaousikia katika vituo vya redio na luninga.
Muziki wa Bongo Flava hauwezi kuisaidia jamii kama wasanii wenyewe wataendelea kuimba imba vitu visivyo na kichwa wala miguu. Mambo hayo tuwaachie wa- magharibi ambao walishatuibia siku nyingi, wamesahau kama kuna mtu katia dunia ya leo, anaweza kuamka asijue wapi pa kuanzia katika kuusaka mlo wa mchana! Kama hawana shida hiyo, hata ukiimba upuuzi wowote watakuelewa, maana wameshiba!
Nimewahi kumsikia msanii moja akiisifu pombe na maisha ya ngono, nikajiuliza, hivi hana cha kuimba? Anasifu pombe ili iweje, kuwafanya watanzania wajue umuhimu wa ulevi?
Nafikiri hii ndio sababu hatushuhudii wasanii wetu wakifanya vizuri kwenye mashindano kama ya Kora. Hawashindi kwa sababu nyingi. Moja ikiwa ni udhaifu wao wa kuimba mambo yasiyoshahibiana na hali halisi ya Maisha ya Waafrika.
Nawashauri wajifunze kwa wenzao (weusi kama wao) lakini wanajua nini cha kufanya unapotaka kuingia studio. Wanatafiti ni kipi kimepungua katika jamii zao, nini kinahitajika na hivyo kitungiwe wimbo.
Wapo Wagosi wa Kaya, Profesa J, wapo akina Ebo waliojua umuhimu wa Utamaduni wa mwafrika. Hao ni wa ndani.
Nadhani kama hawatakuwa tayari kubadilika, waimbe maisha halisi ya watanzania, waishauri jamii kugeuka fikra, basi tutalazimika kugeukia rekodi za nje, watu kama akina Bob Marley na Lucky Dube wanao ujumbe kwa watu masikini kama sisi.

Maoni

  1. Naona kwenye kichwa cha blogu umesema Watanzania tumrejee mungu tukitaka maendeleo. je mungu huyo ni yupi (allah, yehova, ngai, olodumare, ruwa...). Je ni mungu kwa mujibu wa wahindu, wa-Tao, Mabudha, wakristo, waislamu, wazulu, n.k.? Na kama ni kwa mujibu wa wakristo, wakristo hao ni waluteri, wakatoliki, waanglikana, au wasabato?

    JibuFuta
  2. Bwana Macha,
    Mungu kwa mtazamo wangu ni yuleyule, tunambadilisha sisi. Tunataka kumbinafsisha! Ni yule aliyetuumba wote, kwa nini tunataka awe wa dini fulani tu?
    Sasa haya majina ati Allah, yeova nk, nadhani ni kwa sababu hata lugha zenyewe zinatofautiana kutoka kabila moja hadi jingine.
    Ninachoamini mimi ni kwamba Mungu hata ungemwita nani anabaki kuwa yule yule! Na sidhani kama atabadilika eti kwa sababu kaitwa na Mkristo, Muislamu, Mzulu ama Mbuda!
    Tatizo tulilonalo ni kujaribu kumbinafsisha Mungu awe wa watu wa aina fulani tu. Tusifanye hivyo!
    Kw akusema hayo, nadhani kila moja akimrejea Mungu wa Jina lake basi mambo yataenda bara bara.
    Wala rushwa watamwogopa, hawatakula. Wezi wa nchi wakimwogopa Mungu wao, hawataiba.
    Tukimrejea Mungu, sote kwa imani zetu, tena kwa kikamilifu, tutakuwa na uhakika wa maendeleo yetu wenyewe.
    Au unasemaje Ndesanjo?

    JibuFuta
  3. Mada tamu sana hii ndugu yangu. Nitairejea baadaye hapa na pia kwenye blogu yangu. Nipe muda nifanye mawili matatu. Najua Nkya naye lazima atachangia kwenye mjadala kama huu.

    JibuFuta
  4. Swali la Macha ni gumu sana tena sana. Jibu lilillotolewa ni la kiubabaishaji sana tena sana, labda kama mtoa jibu alikuwa anatania au ana malengo tofauti katika hii mada husika. Mungu huyo ni yupi?, wewe kama sisi unao uhusiano gani na huyo mungu? Si unamuongelea mungu yule yule aliyekuwa akienezwa na Livingstone halafu akampa uwezo na nguvu za kuliona ziwa Tanganyika kabla hata ya wale Waha waliokuwa wakiogelea humo kila siku kuliona ziwa lenyewe!!!!!!. Nadhani mada imelenga kueleweka hivi "Tumrejee Mungu Kwani Sisi ni Duni na Hatustahili na Wala Hatuyahitaji Maendeleo". Mwana mada mmoja ana msemo kuwa "tumekwisha". Naamini kuwa blogu ni nguvu na kama ndivyo hivi inavyotumika naongeza kwamba "tumekwisha kabisaaaaaaa". Labda nisichojua ni gharama gani wanalipwa hadi vitu kama hivi kutokea katika nyakati kama hizi za ukombozi.

    JibuFuta
  5. Usomi ni mojawepo ya uwekezaji mtaji. Kama wanavyowekeza wafanyibiashara, wasomi nao wanawekeza katika elimu. Katika mataifa ya Afrika swala la maarifa haliji kwanza. Linalotangulia ni jinsi ambavyo mtu atakuwa na ukiritimba katika eneo fulani utakaompa ugali wa kila siku.

    mwalimu mwenzako mkenya

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Uislamu ulianza lini?