Changamoto za kuwanyima watoto kufurahia utoto wao
Tunaishi kwenye dunia inayopitia mabadiliko mengi. Mabadiliko haya ya kijamii na kiuchumi, kwa kiasi kikubwa, yamezidisha matarajio tuliyonayo kwa maisha. Ukiacha matarajio mengi tuliyonayo kwetu binafsi, kuna matarajio mengi hata kwa wenzi wetu. Mke, kwa mfano, anatarajia mume awe kila kitu anachokifahamu kuhusu mwanamume. Mume ana kazi ya kuwa mcha Mungu, mtu wa sala, mtafutaji na mchapa kazi hodari, mcheshi, rafiki msikivu, kiongozi bora, baba mzuri na mume mzuri asiyechelewa kurudi nyumbani. Matarajio haya makubwa yana faida zake lakini pia yana upande wa pili unaochanga migogoro mingi katika familia.
![]() |
PICHA: Wikimedia Commons |
Hatuishii kuwa na matarajio makubwa kwa wenza wetu. Tunazidisha pia matarajio kwa watoto wetu kiasi cha kuwanyima fursa ya kufurahia utoto wao. Hebu fikiria mtoto asiyeruhusiwa kufanya makosa. Kila analojaribu kufanya, anapodadisi mazingira yake, anakuwa anatafsirika kama mtoto asiye na nidhamu na adabu kwa watu wazima. Kuna namna sisi wazazi tunafikiri woga na ukondoo ni nidhamu na chochote chenye kuashiria udadisi ni utundu na utukutu. Kwa mazingira kama haya, mtoto anajikuta hana uhuru wa kufikiri kitoto, uhuru ambao kimsingi ungemsaidia kujifunza kulingana na uwezo wake.
“Unaogopaje kulala mwenyewe?”
“Unalia dada mzima? Mdogo wako afanyaje?”
“Mwone! Unakuja kunisemea mimi nifanye nini? Hebu ondoka acha kunidekea hapa.”
Tunayasema haya tukiamini tunamsaidia mtoto kuushinda ule utoto wake, ambao kwa utu uzima wetu tunauona kama ni ujinga. Tunachosahau ni kwamba katika ujinga kuna kujifunza.
Pengine kuna haja ya kuelewa hasara ya kuzidisha mno matarajio. Unajua umezidisha kama unaelewa mahitaji ya mtoto kulingana na umri wake. Kuna umri, kwa mfano, mtoto kumlilia mama anapoondoka ni jambo la kawaida. Kuna umri mtoto asipokuwa mbinafsi anayejitanguliza yeye, hawezi kuja kujifunza ukarimu baadae. Kuna umri mtoto asipochafuka hawezi kuchunguza vizuri. Kuna umri mtoto asipokuwa mwongeaji sana, asipokuwa na maswali mengi, basi huenda keshakata tana ya kujifunza kwako. Kwa hivyo unaona, hoja yangu ni kwamba kutokuelewa anachohitaji mtoto kwa umri wake, kunaweza kuwa kichocheo cha kumkomaza kuzidi umri wake.
Kingine nadhani ni mzazi mwenyewe kuzishindwa hisia zake mwenyewe. Mzazi anakuwa kalemewa na mengi na hana mtu mwingine wa kumshirikisha. Ukishakuwa na upweke wa namna hii rahisi sana kumgeuza mtoto dodoki la kukubebea matatizo ambayo ungepaswa kuyajadili na mtu mzima mwenzio.
“Baba yenu ni mtu katili sana. Jana kasafiri hajanipa hata hela ya kutengeneza nywele.”
“Mnaona mama yenu anachonifanyia? Nimemwomba anisamehe mpaka sasa hajanitamkia msamaha.”
“Mwanangu nakuambia mapema. Usije ukalogwa ukawaamini wanawake.”
Haya ni mambo mazito yanayoweza kuharibu kabisa mtazamo wa mtoto kuhusu ndoa. Kuwabebesha watoto mizigo ya kiutu uzima isiyowahusu kunaweza kuharibu kabisa maisha ya baadae. Kusema haya si kurahisisha maisha. Najua kama mzazi unaweza kupitia mengi saa nyingine unazidiwa. Hata hivyo, naamini, malezi ni pamoja na kuwakinga watoto na masuala yanayowazidi ufahamu wao. Ndicho ninachomaanisha ninapopendekeza kuwaruhusu watoto kuufurahia utoto wao.
Kingine, nadhani, ni tabia ya sisi wazazi kutokuuzingatia ukweli wanaoupita watoto wetu. Hapa naomba usome taratibu. Usiwe na haraka. Nguvu kubwa wanazolazimika kuzitumia kuukana ukweli wao wanaojua fiika utawagombanisha na watu wanaowaogopa, watu wanaowahitaji na kuwaheshimu (hapo kwenye watu weka sisi wazazi wao), hutengeneza sura wanayojua sisi wazazi tunaitarajia kwao lakini wakati huo huo ikiambatana na mgandamizo mkubwa wa hatia, fadhaa, hofu, fedheha wasiyoweza kuikiri wazi wazi.
Kadri msokoto huu wa hisia hasi unavyojiimarisha ndani yao, ndivyo wanavyozidi kujibebesha mzigo mzito wa kupambana na jinamizi la matamanio hewa wasiyoweza kuyatimiza kwa hofu ya kukataliwa, kuumizwa, kukosolewa, kuhukumiwa na hata kudharauliwa.
Mpambano huu wa taswira bandia wanayojaribu kuijenga mbele za watu dhidi ya uhalisia wanaotaka kuuishi ndio unaowanyang’anya furaha na utoshelevu wao, ndivyo unavyowakwamisha kuutumia vyema uwezo uliomo ndani yao, na hivyo kuchochea magonjwa mengi yanayozisumbua nafsi zao—ikiwa ni pamoja na sonona. Sijui kama nimejieleza ipasavyo lakini ni ukweli kwamba kuna saa tunawatesa mno watoto kwa kuwazalimisha kuuishi uhalisia wetu enzi hizo unaopingana na uhalisia wao wa sasa. Mifano naomba nisitoe.
Tuwasaidie watoto kujinasua na mtego huu hatari wa kutafuta kukubalika na wazazi wenye masharti mengi, kuwaridhisha wazazi wanaotafuta makosa ili kurejesha upya changamko, uhai, afya ya nafsi zao kadiri wanavyoendelea kukua. Hiki ndicho ninachomaanisha ninapopendekeza kutokuwanyima watoto kufurahia utoto wao.
Maoni
Chapisha Maoni