Hulka ya Mwanadamu Kujikweza na Kukwepa Wajibu
Umewahi kujiuliza kwa nini mtu akifanikiwa jambo (biashara, kazi, elimu, siasa nk) anataka aonekane ana bidii, ana uwezo na kitu cha tofauti kinachomtofautisha na wengine? Kwa nini, kwa mfano, ikitokea kinyume, mtu akashindwa, akafanya vibaya, hutaka ionekane kuna watu wanamkwamisha, kuna upinzani, kuna wabaya wake na inakuwa nadra kukubali huenda tabia zake mwenyewe zinamgharimu?
Mwaka 1978, washunuzi Berglas na Jones waliwatumia wanafunzi wa chuo kuichunguza dhana hii. Makundi mawili ya wanafunzi yalipewa 'puzzle'— fumbo linalohitaji akili kulifumbua. Kundi A walipewa fumbo rahisi. Halikuhitaji kufikiri sana. Kundi B wakapewa fumbo gumu (lisilowezekana hata ukeshe nalo). Makundi yote yalipewa maelekezo kuwa wakihitaji kuboresha uelewa ili wafumbue fumbo wanaweza kuomba kidonge kinachoitwa Actavil lakini wakiona wanahitaji kidonge cha Pandocrin kinachopunguza uelewa pia wangeweza kuomba. Wakati zoezi kiliendelea, 80% ya washiriki wa kundi A (wenye fumbo rahisi) waliomba kidonge cha Actavil (huenda wakilenga kufanya vizuri zaidi) wakati huo huo 19% ya kundi B (fumbo gumu) waliomba kidonge cha Pandocrine. Mara tu ya zoezi kukamilika, mtafiti aliyapa makundi yote mrejesho mzuri kuwa wote wamefanya vizuri sana (wakati ukweli ni kuwa kundi B walishindwa kabisa kufanya chochote). Kisha baada ya pongezi hizo, makundi yote yalipewa mafumbo mengine na kukumbushwa kuwa wangeweza kuchukua vidonge wanavyovihitaji ili wakati wakiendelea na shughuli. MATOKEO: 35% pekee ya kundi A (ambao awali walikuwa wamefanikiwa kufumbua fumbo na kupewa mrejesho kuwa walifanya vizuri) waliomba kupatiwa kidonge cha Activin. Jambo la kushangaza kwenye kundi B (waliokuwa wameshindwa kabisa kufumbua fumbo la awali lakini wakadanganywa kuwa wameweza) 75% WALIOMBA KIDONGE CHA PANDOCRINE!!!
Swali la kujiuliza hapa ni kwa nini jamaa hawa wa kundi B walioteseka mwanzoni na fumbo lisilowezekana waliona bora kuomba kidonge cha Pandocrine ili waendelee kushindwa fumbo linalofuata wakati wenzao wa fumbo A waliokuwa wamefanya vizuri awali hawakuona haja ya kidonge cha kuongeza uelewa? Uchambuzi ulionesha kijinsia wanaume ndio wengi waliomba kidonge cha kushindwa kuliko wanawake. Kuna nini hapa? Ndio uone binadamu tulivyo. Tunapenda tukifanikiwa tuonekane tumepambana, hatujabahatisha na hakuna mchango wa mazingira. Lakini tukishindwa, hatupendi kuonekana tumeshindwa. Haraka tunatafuta visingizio kuhalalisha kushindwa —kishunuzi #SelfHandcapping. Unajitia kwenye mazingira yanayorahisisha maelezo ya mkwamo wako. “Shetani alinipitia.” “Kuna nguvu za giza.” “Nimetoka kwenye familia duni.” “Tulitawaliwa kwa miaka mingi.” Kama kuna tabia tunahitaji kupambana nayo ni hii ya kukwepa kuwajibika matokeo yanapoonesha tumekosea. Kwa upande mwingine, tunapofanikiwa ni muhimu kuwa wanyenyekevu na kuukubali ukweli kuwa pamoja na jitihada zetu, kuna bahati, watu, mazingira na sababu nyingine zilizo juu ya uwezo wetu. Tusipojifunza haya mawili, kwa hakika, tutakuwa tunajidanganya. Rejea: Berglas, S., & Jones, E. E. (1978). Drug choice as a self-handicapping strategy in response to noncontingent success. Journal of Personality and Social Psychology, 36(4), 405–417.
Maoni
Chapisha Maoni