Nani Awezaye Kutuletea Mabadiliko Tunayoyataka?
Ukisikiliza mazungumzo ya
wa-Tanzania –iwe vijiweni, mitaani,
mitandaoni ama kwingineko –ni wazi wengi wetu tunayo hamu ya mabadiliko. Tuna shauku
ya zama mpya. Shauku hiyo ya mabadiliko imetufanya wengi wetu tutumie muda
mwingi kutafuta watu tunaohisi ‘wanatukwamisha.’ Ni hivyo kwa sababu
tumejijengea dhana kwamba ili kupata mabadiliko tunayoyataka tunahitaji watu maalum
wenye uwezo wa ‘kutuletea maendeleo’. Kwa hiyo ni kama tunasubiri wakombozi fulani
fulani waje kutubadilishia mfumo tunaoamini ndio tatizo.
Mfumo ni nani?
Wananchi wengi tunapozungumzia
mfumo tunafikiria ‘yanayofanywa na wenye mamlaka ya kutuletea maendeleo/mabadiliko.’
Tunafikiri tatizo letu kubwa ni watu wengine na hivyo mara zote tunajiweka
upande wa kuwalaumu. Tunadhani ikiwa wengine (wenye mamlaka) wangefanya yale tunavyotamani
yafanywe basi hali ya mambo ingebadilika. Kwa hiyo mara zote tunakuwa na orodha
ndefu ya watu wa kuwanyooshea kidole isipokuwa sisi wenyewe.
Kwa mfano, mwalimu anapofelisha
wanafunzi wake analaumu ‘mfumo wa elimu.’ Anatumia nguvu nyingi kuthibitisha
kwamba tatizo haliwezi kuwa yeye bali watu wengine anaowaita mfumo. Kwake, tatizo
ni mitaala isiyofaa, serikali isiyofanya wajibu wake, wanafunzi wasio na sifa
na kadhalika. Analaumu wengine.
Ndivyo tunavyojadili matatizo
yetu. Kila anayeshindwa kufikia matarajio ya jamii au anayedhani mambo hayaendi
ipasavyo jibu ni jepesi: mfumo. Wananchi (tunaoitwa wa kawaida) tunashinda
vijiweni ‘kuchambua’ namna siasa zetu zinavyoturudisha nyuma. Tunatumia masaa
mengi kuwalumu watu tusiowajua. Tunaishi kwenye mazingira machafu lakini
hatuchukui hatua kwa sababu ‘mfumo’ wa kusafisha takataka zilizotapakaa kwenye makazi
yetu haufanyi kazi. Tunasubiri ‘mfumo’ uje utuzolee takataka zinazoathiri
maisha yetu. Tusipowaona ‘watu wa mfumo’ wanaoweza kutupa matumaini ya kutatua
matatizo yaliyo ndani ya uwezo wetu basi tunakata tamaa.
Hatuwezi kuchukua hatua zilizo
ndani ya uwezo wetu?
Natambua umuhimu wa hicho
tunachopenda kukiita mfumo. Natambua umuhimu wa viongozi wetu kuongoza harakati
za kuhamasisha utatuzi wa changamoto zinazotukabili. Hata hivyo, pamoja na
umuhimu wa mfumo, napendekeza sisi wananchi kutambua umuhimu wa kuchukua hatua zilizo
ndani ya uwezo wetu kuleta mabadiliko tunayoyataka. Tubadilike.
Kuchukua hatua maana yake kabla
ya mwalimu kulalamikaia mfumo wa elimu, ajiulize yeye amefanya wajibu wake
ipasavyo? Amejibidiisha kutatua changamoto za wanafunzi zilizo ndani ya uwezo
wake? Kama mwalimu anashindwa kushughulikia matatizo madogo yanayowazuia angalau
wanafunzi wake kumi kuelewa somo lake, anawezaje kuzungumzia matatizo ya mfumo
wa elimu wa nchi nzima? Kwa nini, kwa mfano, kwa kushirikiana na uongozi wa
shule, kijiji na kata anamoishi, asijenge mfumo unaweza kufanya kazi darasani
kwake? Hili haliwezekani?
Wananchi wakishiriki kusafisha mazingira yao. Picha: wazalendo25.blogspot.com |
Ukweli ni kwamba kila mwananchi
anaweza kuleta mabadiliko anayoyataka ikiwa atatambua na kutimiza wajibu wake
kikamilifu. Hili linahitaji kubadili mtazamo. Kwa kubadili mtazamo na kuamua
kuanza kuchukua hatua badala ya kutafuta makosa ya wengine, tunaweza kuleta
mabadiliko. Hatuwezi kubadili chochote kwa kushinda kwenye mitandao ya kijamii,
vijiweni, korido za maofisi kulalamikia watawala tunaowaona kwenye televisheni.
Tunaweza kuleta mabadiliko makubwa kwa kila mmoja wetu kutambua mchango wake
katika kuleta tofauti anayoitaka.
Viongozi wetu wa mitaa/vijiji/kata
tunawajua na tunaweza kuwafuatilia kwa karibu. Tunaweza kushirikiana nao kufikiri
namna bora ya kujenga mfumo utakaofanya kazi kwenye maisha yetu halisi. Sote
kwa pamoja kuanzia chini tunaweza kushirikiana kujenga vimfumo vidogo vidogo
vya kubadilisha hali ya mambo katika maeneo tunayoishi. Tukifanya hivyo, tutarahisisha
kazi ya wale tuliowapa dhamana ya kujenga mfumo wa kitaifa utakaoakisi mifumo tuliyojenga
sisi wenyewe kuanzia chini. Hayo ndio mabadiliko ya kweli. Mabadiliko ya
mtazamo.
Twitter: @bwaya
Maoni
Chapisha Maoni