Unavyoweza Kumsaidia Mtoto Kuwa Mkweli
Bila shaka umewahi kujiuliza kwa nini mtoto amekudanganya kwa jambo dogo ambalo, kwa hali ya kawaida, angeweza kukwambia ukweli na mambo yakaisha. Chukulia kwa mfano, una watoto kadhaa nyumbani. Unagundua kuna kosa limefanyika. Unapowauliza kujua nani aliyehusika, hakuna anayekuwa tayari kukubali. Kama umekuwa ukijiuliza kwa nini watoto hudanganya, usiwe na wasiwasi. Karibu watoto wote hudanganya katika mazingira fulani fulani. Wanapodanganya, hata hivyo, nia yao huwa ni kulinda uhusiano wao na wewe mzazi kwa kusema kile wanachojua unakitaka. Tahadhari ni kuwa ikiwa kudanganya kwa nia njema kutaachwa kuendelee, hujenga tabia ya uongo mbeleni.