Machapisho

Inaonyesha machapisho kuanzia Novemba, 2007

Hitilafu ndogo

Kutokana na sababu ambazo ni za wazi, ili kublogu huwa natumia tarakilishi-paja kuandikia na kisha kuja mtandaoni kupesti maandiko yangu. Kufanya hivyo hunipunguzia gharama za muda wa kukaa mtandaoni ambao kwa nchi tajiri kama yetu, unagharimu sana. Kwa bahati mbaya sana, tarakilishi hiyo imepata UKIMWI siku kadhaa zilizopita! Kuna kirusi kaivamia na ananizuia kufanya chochote. Jitihada za kumtafuta daktari wake zinaendelea.

Kuwa halisi, ufe halisi

Kila binadamu anazaliwa halisi/origino. Uwezo halisi. Akili halisi. Mtazamo halisi. Maono halisi. Sura halisi. Machache kwa kutaja. Uhalisi huu una maana ya kuwa na uwezo wa kipekee katika uasili wake ili kutimiza jukumu halisi na la kipekee katika jamii. Bahati mbaya idadi kubwa ya wanadamu hawa waliozaliwa origino, wanakufa wakiwa "fotokopi" za watu fulani. Wanaiga kila kitu. Mtizamo bandia. Fikra bandia. Akili bandia. Uwezo bandia. Sura bandia. kazi bandia. Na kadhalika. Bandia hapa ina maana ya kuwa ama kujaribu kuwa mtu mwingine tofauti na yule halisi aliyezaliwa akiwa wewe. Bandia ina maana ya kutafuta kufanya jambo lisilo lako. Kuiga. Kupoteza muda kufanya kitu ambacho si halisi yako. Vipi, u halisi wewe? Au umekuwa fotokopi ndugu yangu? Rudi kwenye mstari utafute uhalisi wako. Hapo utakuwa umejielewa.

Tubadilishe mfumo wa kufikiri

Hivi ingekuwaje kama tungeweza kuutumia ubongo wetu walau kwa asilimia chache za uwezo wake halisi? Hivi ingekuwaje kama kila Mtanzania angeamua kuacha uvivu na kuzifanyia kazi baadhi tu ya seli mabilioni zinazounda ubongo wake? Tungebaki hapa tulipo? Nina mashaka iwapo kila raia wa nchi hii anajisumbua kujua matumizi sahihi ya ufahamu wake. Kila raia naamini anayo akili nzuri ambayo kama ikitumiwa kwa kiwango kizuri lazima isababishe mabadiliko ya aina fulani. Na tunapozungumzia akili nzuri, haturejei kwa wale wachache waliobahatika kuyakanyaga madarasa. Kama hivyo ndivyo, kwa nini tunaendelea kurudi nyuma kwa kasi mpya? Kwa nini tuna mazoea mabovu ya kulalamikia mambo ambayo wakati mwingine ni sisi wenyewe tumeyasababisha? Hivi kweli tunatumia akili zetu ipasavyo? Sababu imekuwa kawaida kusikia malalamiko. Watu tunajua kulalamika. Na kulalamika maana yake ni jitihada za kukwepa majukumu kwa kuwatupia wengine mzigo ambao kimsingi ni wa kwako. Kulalamika ni kule kushindwa kukubali ud

Acha woga, zaa mawazo

Leo naamkia uzazi. Uzazi wa mawazo. Mawazo. Mawazo. Upo umuhimu mkubwa sana wa sisi kama binadamu kujielewa. Kujielewa kutatusaidia kutatua matatizo yetu mengi. Matatizo ya kiutamaduni. Kisiasa. Kijamii. Na kadhalika. Kulielewa ni muhimu sana. Kujielewa ninakokuzungumza hapa ni kule kufahamu kuwa ndani mwako yapo mawazo ambayo usipoyagundua yatakufa na wewe. Wewe unayo mawazo muhimu sana kwa ajili ya maendeleo ya watu wanaokuzunguka. Bahati mbaya ni kwamba mawazo hayo yanakusubiri wewe uache woga. Useme. Ueleweke unawaza nini. Mengi ya matatizo yetu hayako huko tunakodhani. Si unajua mara zote huwa hatupendi kuwajikia matatizo? Chanzo cha matatizo yetu kiko katika fahamu zetu wenyewe. Lakini ajabu ni kwamba watu wengi tunajua sana kuzungumzia udhaifu wa wengine. Tunajua kuchambua hoja za wengine. Tunajua kupuuza vya wengine. Tunajua kulalamika. Kusononeka. Lakini kumbe kufanya hivyo hakuwezi kuleta mabadiliko ya kweli. Hivi sasa wananchi wanalalama. Serikali imefanya hiki. Serikali. Se

Ni kujielewa si kujitambua tena

Haya. Nilipotea. Kwa vigezo vyenu nakubali. Sasa nimerudi. Kurudi kwangu kumekuwa kwa jina jipya. Blogu hii tuliita Jitambue lakini baada ya kupitia pitia kumbukumbu, tukafahamu kuwa ipo blogu ambayo inaitwa kwa jina hilo ingawa imekuwa mapumzikoni tangu elfu mbili na tano. Hatujui itarejea lini ila tunaamini itarejea. Sasa ili kumrudisha ukumbuni mwenye blogu hiyo, tumeona ni vyema sisi wa hapa tujitambulishe kwa jina jingine ambalo maana yake inabaki kuwa ni ile ile. Mengi ya maudhui yetu yatakuwa yamejikita katika kujielewa. Tutajaribu kuzungumza kwa muhtasari sana habari ya sisi kama binadamu kujielewa wenyewe kazi ambayo ni muhimu sana. Watu wengi wamekuwa na kazi ya kuelewa mambo mengine, wakati wao wenyewe hawajijui. Tunadhani kwamba kuyaelewa mambo mengi bila kujielewa mwenyewe ni hasara na kujilisha upepo. Unapotembelea blogu hii, usitazamie kusoma siasa. Kwa sababu siasa haikusaidii kujielewa. Tazamia kusoma maswali yanayoweza kukufanya uongeze tafakari kukuhusu wewe mwenyewe

Nini maana ya muda?

Kuna rafiki yangu mmoja kanitumia ujumbe mrefu wa barua pepe akinipa vidonge vyangu kwa kuitelekeza blogu hii kwa muda mrefu. Yeye hana blogu, ila ni mfuatiliaji wa wenye blogu akifatilia yupi yuko wapi ana ansema nini. Basi, kupata ujumbe ule kunanikumbusha nadharia ya muda (kosmolojia): Muda ni nini hasa? Unaposema muda unaenda, unamaanisha nini hasa? Ili kujibu vidonge vya huyo rafiki yangu huyo hebu tuone muda maana yake nini. Muda unatokana na mabadiliko. Huwezi kuhesabu muda kama hauna mabadiliko. Dunia inahesabu masaa kwa sababu kuna mabadiliko. Inakuwa mchana inakuwa usiku. Inakuwa kiangazi inakuwa masika. Mabadiliko. Yasingekuwapo mabadiliko hayo pasingekuwapo na kitu kinachoitwa muda. Aidha, muda unatofautiana kati ya desturi na desturi, mtu na mtu, kazi na kazi na kadhalika. Kwa mfano, kwa mtu alikufa kwake muda ni sifuri kwa sababu mwili wake hauna mabadiko ya aina yoyote kwa vigezo vya kiumbe hai. Na pia katika jamii ambamo mabadiliko ni ya haraka, kwao muda unakuwa mdogo.

Wewe ni nani?

"Wewe ni nani?" Uliza swali hili kwa kila unayekutana naye na sikiliza majibu yao: "Mimi ni Idi" "Mimi ni Mashaka" Tena kwa kujiamini kabisa. "Mimi ni Masumbuko" Huku akikushangaa kwa kumuuliza swali la kitoto. Ukionesha kutokuridhika na majibu hayo mepesi, ukaongeza swali jingine, sana sana utaonekana mtu wa ajabu unayeuliza kitu kinachoeleweka. Utaonekana huna kazi. "Unaulizaje swali kama hilo? Ina maana unataka kunifanya mimi sijijui?" Lakini ukweli ni kwamba pasipo kujibu swali hilo, kila unachokifanya kitakuwa ni kupotea njia. Sababu wewe ulikuwa wewe kabla hujapewa hilo jina ulilonalo. Yaani wewe ulikuwa wewe kabla hujaambiwa ni wewe. Jitahidi usipotee njia. Anza leo. Jijibu swali hilo. Nakutakia siku njema ambayo inaweza kuwa mwanzo wa kujua wewe ni nani hasa wakati unazaliwa.

Jua furaha yako iko wapi, itafute

Tofauti ya binadamu na viumbe wenzake wote, iko katika ufahamu. Binadamu anaweza kutumia ubongo wake vizuri zaidi na hivyo kujitofautisha na "wanyama" wenzake wasiojua wanakotoka na wanakoelekea. Anao uwezo wa kujua anataka nini na afanyaje kukibapata. Wenzake wote, pamoja na Sokwe mwenye Di Eni Ei zinazokaribia kufanana na zake, na hata wengine tukadhani wanachangia babu wa babu, hawana kingine wanachokitafuta zaidi ya uzazi. Wao, kuzaa kunamaana ya kufikia kiwango cha juu cha mafanikio katika kipindi cha maisha yao. Wakishazaa basi, hata wakifa, kwao kifo hicho hakitahesabika kuwa cha hasara. Nini kusudi la binadamu kuzaliwa? Je, binadamu huyu anatafuta kitu gani katika kipindi cha maisha yake ambacho akikipata hicho basi anaridhika? Anataka nini ambacho akiisha kukipata basi, kwake hayo ndiyo mafanikio katika kilele chake? Je, ni kuzaa kama ilivyo kwa ndugu zetu wanyama? Je, ni kuwa na mke mrembo kuliko wote (kama kweli yupo)? Ni kuwa bilionea nambari moja Bongo yote? Ama