Kwa nini uko hivyo ulivyo?

Bila shaka umewahi kuonana na watu wenye aibu. Huenda na wewe unalo tatizo hilo la aibu. Au unamfahamu binadamu mwenye tatizo la mkono wa birika. Ama watu wenye mtazamo hasi tu katika kila kitu. Wenye kuwaza ubaya tu kwa watu wengine. Au pia inawezekana umewahi kuwaona watu wenye kupenda ngono utafikiri chakula na chai ya asubuhi. Na vijitabia vingi vingi hivi ambavyo hutokea hatuvipendi ila tunavyo.

Ningependa tujadili chanzo cha tabia hizi na namna ya kuachana nazo. Ninajaribu kurahisisha maelezo ya kisaikolojia katika lugha nyepesi ili kuona namna ya kushughulikia matatizo-nafsi kwa namna rahisi zaidi.

Ukweli ni kwamba kila mtu ni mwana-saikolojia. Hata kama wapo wanadhani kujua saikolojia ni mpaka ukasugue dawati darasani kwa miaka kadhaa lakini bado ukweli uko pale pale kwamba wewe ni mwana-saikolojia. Labda utadhani natania. Hebu fikiria, ni mara ngapi umeweza kubaini kuwa mtu fulani hana furaha ama ana huzuni ama amekasirika na kadhalika? Umejuaje?

Unapoweza kujifunza kinachoendelea katika ufahamu wa mtu, ukajua kinachosababisha awaze hivyo anavyowaza, ama awe na tabia hizo alizonazo, basi unajihusisha moja kwa moja na elimu-nafsi ama saikolojia katika urahisi wake.

Kuna ukweli fulani kwamba tabia ulizonazo zimetokana na mambo mengi. Tabia yako ni zao la muunganiko wa vibeba urithi kutoka kwa baba na mama yako, vilivyobebwa katika mbegu na yai vilivyoungamana kukutengeneza wewe. Hiyo moja. Lakini pili, ni zao la mwingiliano wako na mazingira yako.

Dhana ya mazingira hapa inaanzia na watu unaoishi nao kwa karibu mfano wazazi wako, yaya aliyekulea, watoto wenzio na kuendelea mpaka hata mambo kadha wa kadha uliyokumabana nayo tangu ukiwa tumboni mwa mama yako. Vyote hivyo katika ujumla wake, vimeshiriki katika kukutengenezea tabia uliyo nayo leo.

Tabia yako ni mjumuisho wa mawazo yaliyoruhusiwa ama kujiruhusu yenyewe kujibanza katika ufahamu wako na hatimaye kujidhihirisha katika mwenendo unaoonekana. Hivyo basi twaweza kukubaliana kimsingi kwamba tabia yako hukuzaliwa nayo ila imejitokeza kama udhihirisho wa namna ulivyokuzwa na mazingira yako iwe watu ama hali/matukio kama tulivyogusia hapo awali.

Nafasi kubwa ya ujenzi wa tabia yako imechezwa na watu uliojikuta kati yao mara tu ulipozaliwa na ukaendelea kuishi nao kwa muda mwingi katika miaka ya mwanzo ya maisha yako. Watu hawa kwa tuliowengi, ni wazazi wetu.

Miaka ya mwanzo ya ukuaji wako, ndiyo hasa kwa sehemu kubwa imechangia wewe kuwa kama ulivyo leo hii. Sababu ni kwamba ufahamu wako ulikuwa kama kaseti tupu iliyokuwa na kazi moja ya kurekodi kila kinachotokea, kazi ambayo huenda hukuweza kuigundua sababu ubongo wako ndio hasa ulihusika.
Wazazi ni watu muhimu sana katika ujenzi wa tabia za watoto wao. Kama ambavyo mbegu za uzazi ndizo huungana kutengeneza kijusi ambacho huja kuwa mtoto, ndivyo ambavyo malezi na mwenendo mzima wa maisha katika nyumba yao hutenegenza tabia za aina yoyote kwa watoto wao.

Ukiondoa tofauti ndogo ndogo, watoto wote wangeweza kuwa na tabia moja ikiwa wangekuzwa katika mazingira yanayofanana. Tofauti ya tabia tunazoziona leo, zinatokana na tofauti ya malezi/mazingira baina yetu.

Kuna wazazi , hasa wanaume, ambao hujiona kuwa na mamlaka yasiyo na mipaka kiasi kwamba wanayo hiari ya kuamua chochote nyumbani pasipokusikiliza wengine. Ni madikiteta wanaoweza kuwakunjia ndita wake zao mbele ya watoto wao. Na ikibidi kwa kufoka foka kwa sababu wanayo orodha ndefu ya madai kwa watu wengine kuliko wanavyotoa wao. Mara nyingine, hata katika mambo yanayomhusu mtoto mwenyewe moja kwa moja, bado wanaendesha udikteta kwa amri zisizohojiwa.

Wapo wazazi ambao ni wagumu katika kuwasifu watoto wao pale wanapofanya jambo fulani kama ilivyotakiwa. Kwao, mtoto hata siku moja hawezi kufanya kitu sahihi na kwamba hastahili pongezi kwa chochote. Na hata anapofanya vyema, huo ni wajibu usiostahili pongezi. Kwa lugha nyepesi wanamchukulia mtoto kama kifaranga fulani hivi.

Wazazi wengine ni wanasheria-ngumu. Kila kitu sheria. Kuvaa sheria. Kulala sheria. Kula sheria. Kuoga sheria. Sheria sheria sheria. Na sheria zenyewe zimeundwa pasipokumshirikisha huyo anayetungiwa sheria. Kinachohitajiwa ni utekelezaji full stopu! Pengine ulikulia katika malezi ya namna hii ama na wewe ni mzazi wa sampuli hii.

Tabia za watoto, zinatupa habari za udhaifu ama ubora wa malezi ya wazazi husika. Kwa maana rahisi kila mtoto anatengenezewa tabia na wazazi/mzazi wake. Mkandarasi wa tabia zangu kwa kiasi kikubwa ni mzazi wangu. Injinia wa sehumu kubwa ya tabia yako ni mzazi wako. Na tuangalie kwa kifupi.

Ikiwa wazazi walikuwa na na aina ya malezi ya sheria ngumu ngumu, wakikushurutisha kufanya mambo bila hiari yako, ni wazi kuwa ufahamu wako ulijenga dhana ya kutokujiamini kwa maana ya kwamba eti wewe si aina ya mtu awezaye kufanya kitu na watu wakakikubali. Matokeo yake unakuwa mtu anayejishuku kwa kila unalolifanya ukijiuliza uliza sana jinsi watu wanavyokuchukulia. Ndio maana ukisimama mbele za watu unashindwa kujiamini kwa sababu ya kufikiri zaidi hadhira hiyo inakuonaje. Ninazungumzia aibu.

Pengine nyumbani kwenu mtindo ulikuwa kila ukipendekeza jambo, baba yako alikukemea. Ukaogofywa. Kila ulipofanya kitu wazazi wako hawakuonyesha kukitambua, na waliishia kukulaumu tu hata kwa makosa amabyo twaweza kusema ni ya kawaida. Pengine siku moja ulifua nguo ukaianika. Mama yako kwa kujua kuwa haijatakata, akaianua na kuipiga sababu upya huku wewe ukishuhudia udhalilishwaji wa namna hii! Ukajiuliza mwenyewe imekuwaje anairudia wakati uliifua vizuri kwa mujibu wa kiwango cha udobi wako? Moja kwa moja dhana ya kwamba huwezi kufanya kitu kama kitakiwavyo ikachukua nafasi yake.

Inawezekana wazazi wako walikuwa na tabia ya kuficha sana vitu hasa vile walivyoviona kuwa ni vya thamani. Na kwa sababu kama mtoto ulitamani kuvipata. Basi ikakubidi mara nyingine, utumie akili ya ziada kutimiza nia yako hiyo, pasipo wao kubaini. Ukaanza udokozi. Kulamba sukari. Kudokoa minofu jikoni. Kupiga simu iliyotiwa kufuli kwa kutumia kijiko. Na mifano mingine. Matokeo yake ufahamu wako ukajenga hoja kuwa: Haiwezekani kuvipata vitu vingine pasipo kutumia mlango wa uani. Sababu ni kwamba ukivitaka kwa halali utangoja mpaka liamba, kamwe hutavipata. Taratibu unaanza kujenga tabia ya wizi.

Pengine wazazi wako hawafanikiwa kukuaminisha kuwa wanakupenda. Hata kama walikupenda, waliogopa kukuonyesha waziwazi, wala hawakukutamkia. Inawezekana waliamini huhitaji sana upendo wao wa waziwazi. Basi ukakua ukikosa hitaji la kupendwa. Ongeza ukali wao. Kutiwa viboko bila maelezo ya kosa. Kutokupatiwa mahitaki yako, ndio kabisa ukatia muhuri kwamba wazazi wako wanakuchukia.

Bahati mbaya rafiki zako ndio ukawaamini kuliko wazazi wako kwa sababu wanaonyesha kukujali na kukupenda. Moja kwa moja unajikuta ukiwasikiliza wao na ushauri wao kuliko “zilipendwa” za wazazi wako. Ongeza balehe. Mwili unakutuma kuhusiana na jinsia ya pili. Halafu katika mazingira hayo, unapata jinsia ya pili inayojua kutamka bila kusita kwamba inakupenda. Na kwa sababu jamii yetu inaamini “ kama unampenda hutamnyima” kwa maana ya kwamba hakuna mahusiano pasipo ngono, na kwa sababu kupendwa ni hitaji la kila binadamu, basi kwa vyovyote vile iwavyo, wazazi wako watakuwa wamechangia. Na ilivyo ajabu ni kwamba ndio hao hao watakakuja juu wanapobaini kuwa binti yao sasa hivi ana mahusiano ya hovyo na mkata majani wa jirani.

Changamoto ninayotaka kukuachia wewe uliye mzazi, ni kujiangalia upya, kwa kuwatazama wanao walivyo. Hapo utakuwa unajihukumu mwenyewe, kwamba ni kwa kiasi gani umefanya ulio wajibu wako kama mzazi. Usiishie kulaumu kona za barabara, unasahau kuwa mkandarasi wa barabara hiyo ni wewe.

Maoni

  1. kuna vitu viwili vinavyochangia tabia na uwezo au haiba ya mtu.Navyo ni Asilia(yaani Nature )na mazingira(yaani nurture).Kila binadamu anazaliwa na uwezo fulani(potential)lakini ili uwezo huo ufikie kiwango chake cha juu(maximum potential) basi lazima kuwepo na mazingira yanayoruhusu ukuaji huo.Lakini pia asilia au mazingira huweza kuweka kipingamizi(limitation)dhidi ya uwezo wa mtu.Kwa mfano hata mtu apate mazingira mazuri namna gani kama hana asili ya urefu(yaani genes for tallness) mtu huyo hawezi kuwa mrefu.mada hii bado ni moja ya gumzo(an issue) katika saikolojia na hivyo waandishi wa sasa wanakubaliana na usemi kuwa yawezekana tabia au uwezo wa mtu huchangiwa na asili(nature) ya huyo mtu kupitia (via) mazingira(nurture).majadiliano baina ya wataalaam yanaendelea.

    JibuFuta
  2. Shehe Yahya anasema kuwa tuko hivi kutokana na mpangilio wa nyota na sayari angani wakati tulipozaliwa:)

    Unasemaje?

    JibuFuta
  3. Kama kuna vitu huwa vinanishangaza. basi unajimu ni mmoja wapo. Sijajielimisha sana kuhusiana na elimu hii. Labda kama unafahamu naomba kuuliza: Huo mpangilio wa nyota na sayari wanaouzungumzia, unahusikaje na namna tulivyo? Ina maana kila mtu anayo nyota yake angani inayodhibiti mtazamo na hulka yake?

    Halafu inakuwaje, kwamba unapozaliwa tarehe fulani basi uhusishwe na tabia fulani fulani? Kuna uhusiano gani kati ya siku anayozaliwa mtu na tabia yake?

    JibuFuta
  4. Nimeona watu ambao wamezaliwa kipindi kinachofanana lakini wenye tabia tofauti zisizoshahibiana. Sina hakika kama wanajimu kama Shehe Yahya wanakuwa sahihi kuhusianisha tabia zetu na mambo ya nyota. Vinginevyo tunahitaji kupata elimu hiyo pia.

    JibuFuta
  5. Kuna mtu kanitumia blogu yako akisema kuwa huu ni mfano mzuri sana wa kazi nzuri za kuelimisha za wanablogu. Nami nakubaliana naye.

    JibuFuta
  6. NDIO KUNA WALE WANAOSOMEA SAIKOLOJIA WANAMFAHAMU MTU KIUNDANI ZAIDI JE NI KWELI KUNA WATU WANAATHIRIKA KISAIKOLOJIA HASA KAMA ANA MPENZI WAKE NA AKAPA EFFECT KUTOKANA NA MAPENZI

    JibuFuta
    Majibu
    1. Yes wapo kutokana na Hali yakuwa na uwezo mdogo wakuzikabili changamoto katika mahusiano yenu

      Futa
  7. Kiukweli naelimishwa mengi sana kupitia blog hii ,kilichozungumziwa hapa kinanigusa na kinanifudisha pia.

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Uislamu ulianza lini?