Mbinu za Kumfundisha Mtoto Kusoma Akiwa Nyumbani
Katika utafiti uliofanywa na program ya Uwezo iliyochini ya Shirika la Twaweza, zaidi ya nusu ya watoto wa darasa la nne na tano katika nchi za Afrika Mashariki hawana uwezo wa kusoma na kuandika. Nilimwuuliza Bahiya Abdi, mhadhiri wa masuala ya mitalaa, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge, maana ya kutokujua kusoma na kuandika. Anasema: “Kuna mambo kadhaa ya kuangalia tunapozungumzia uwezo wa mtoto kusoma. Mbali na mtoto kutambua herufi, lazima awe na uwezo wa kusoma kwa haraka.” “Lakini pia, uwezo wa kusoma unapimwa kwa kiwango cha kuelewa kile anakisoma. Kama mtoto anaweza kusoma tu lakini hawezi kupata ujumbe vizuri, hapo tunaweza kusema uwezo wake uko chini ya kiwango.” Kwa mujibu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TIE) mtoto wa darasa la kwanza na la pili anatarajiwa kutambua na kusoma kwa ufasaha maneno 50 yenye maana kwa dakika na maneno 40 yasiyo na maana kwa dakika. Kadhalika, anatarajiwa kuandika kwa ufasaha herufi kubwa na ndogo, na kufanya hesabu za kujumlisha na k...