Dunia mbili katika nchi moja?
Nilikuwa nikifuatilia namna watuhumiwa 'wetu' wasiohesabika wanavyopata dhamana. Kweli nchi hii ina mambo. Wakati kila mtuhumiwa anaweza kutoa hati ya nyumba (soma hekalu) lenye kukaribia shilingi za kitanzania bilioni moja, asilimia kubwa ya watanzania waliobaki hawana hata uwezo wa kupata milo miwili iliyotimia kwa siku. Wakati kuna wenzetu wachache (hata kama hawana hatia) wanaouwezo wa kujiwekea dhamana ya mabilioni ya shilingi, idadi kubwa ya watanzania waliobaki hawana hata ndoto ya kujenga pango lenye chumba kimoja. Hali hii inatupeleka wapi watanzania? Dunia mbili katika nchi moja? Kwamba katikati ya umasikini huu, wapo wenzetu wachache wanaoogolea ukwasi wa kutisha? Mabilionea hawa wana raha ipi ikiwa wamezungukwa na mafukara pande zote? Tafakari.