Kutumia UmahiriHisia (Emotional Intelligence) Kuimarisha Mahusiano

Tunamalizia safari yetu ya kujifunza umahirihisia. Tumeangazia maeneo makubwa manne. Kwanza, uelewa wa hisia na sababu zake. Pili, tulitazama namna ya kurekebu hisia zetu . Kisha tukatazama namna tunavyoweza kujenga motisha na hamasa ya kufikia malengo yetu . Kisha tukaangalia namna umahirihisia unavyotuwezesha kuwasiliana na watu pasipokuzalisha migogoro isiyo na sababu. Maeneo haya manne ya umahirihisia, yanatafsirika katika mahusiano yetu na watu —namna tunavyowachukulia wasioamini tunachokiamini, namna tunavyowajibu wasiofikiri kile tunachokifikiri, namna tunavyotatua migogoro na maamuzi tunayochukua pale tunapojisikia kuonewa. Msingi wa mahusiano yenye tija na watu ni uwezo wako wa kujitambua, kutambua namna hisia na tabia zako zinavyoathiri wengine, namna unavyomudu hisia zako lakini pia kiwango chako cha upendo kwa watu. Mtu mwenye #UmahiriHisia hagombani kirahisi. Ukigombana naye anajua namna ya kujinasua na kukuachia ugomvi wako...