Tumefinyangwa kuwa wakimbizi wa kudumu
KADIRI siku zinavyosonga mbele, ndivyo waswahili tunavyozidi kuwa watu tusiojitambua. Namaanisha kutokujifahamu sisi ni akina nani na tunatofautianaje na wasio watu wengine waliobaki katika uso wa dunia. Tunashindwa kuyaelewa mazingira yetu na thamani ya ustaarabu wetu ambao (huenda) ni ushenzi kwa wengine. Badala yake tunageuza ushenzi wao kuwa ndio ustaarabu rasmi wa jamii yetu. Tunashindwa kujua mwelekeo wetu kama watu wenye ustaarabu wao ambao ndio unaoleta maana ya maisha yenye alama ya Utanzania. Matokeo ya haya matatu ni kurudi nyuma katikati ya hayo yanayoonekana kuwa ni maendeleo. Hapo ndipo tunapogeuka kuwa mazuzu wenye vitu ambavyo babu zetu hawakuwavyo lakini bado tukiishi hovyo kuliko hata walivyoishi wao. Kwa maana nyingine, tunakuwa watu wenye “zaidi” kwa habari ya vitu, lakini wenye “ukosefu” kwa habari ya thamani ya kweli ya utu wetu. Swali tunalojiuliza hapa ni iwapo ni busara kung’ang’ania kuyatafuta maendeleo (kwa maana ya vitu na huduma) pasipo kwanza kuubaini ...