Ben Carson: "Mswahili" bingwa Marikani

Afrika imejaa watu ambao wakizitumia mbongo zao ipasavyo wanatikisa kabisa historia ya Dunia hii. Wanatetemesha! Mifano ya waafrika waliosumbua historia yetu ni ndefu. Tatizo letu kubwa ni kwamba hatuwaoni mabingwa wengi walio nje na ulingo wa siasa.

Ben Carson, ni Mmarikani mweusi, daktari bingwa wa Nyurolojia (Neurosurgeon)katika hospitali ya Johns Hopkins aliyewahi kutenganisha mara kadhaa mapacha waliounganika vichwa vyao. Kishawahi kuja Afrika, kuwatenganisha watoto wenye matatizo hayo ambao wanaishi mpaka leo. Ben hutumia masaa mengi kwa siku akifanya upasuaji wa “Mbongo” za watoto hasa wenye matatizo ya uvimbe kwenye ubongo. Bonyeza hapa kupata simulizi zake kwa ufupi. Mtandao wa Topblacks umetambua mchango wake unaoleta heshima kwa weusi wa nchi hiyo. Huyu bwana, pamoja na kuwa Daktari wa Tiba za Afya, ameandika vitabu kadhaa akijaribu kutoa wosia kwa vijana hasa wanafunzi wa shule namna ya kufanikiwa katika masomo. Anao pia mfuko wa kusomesha vijana wanaofanya vizuri. Huu hapa.

Katika kitabu chake cha GIFTED HANDS anaeleza jinsi alivyokuwa mbumbumbu wa mwisho darasani na namna alivyokuja badilika katikati ya ubaguzi wa rangi ya ngozi yake na umasikini uliotopea. Ben anamtaja sana Mama ake Sonya kama mtu aliyemsaidia sana kwa kumlazimisha kuingia maktaba na kujisomea vitabu, shinikizo lililokuja kumsaidia sana na kumjengea tabia ya kupenda “kula vitabu”.

Katika THINK BIG, kitabu chake cha pili, Mwafrika huyu anaelezea falsafa yake anayoiita THINK BIG ambayo inaelezakwa kirefu herufi moja moja katika neno hilo ambayo kwayo, anaamini Ben, kuwa itamsaidia mwanafunzi kuweka mazingira mazuri ya kufanikiwa. Anataja mambo mengi yanayoweza “kumtoa” mtu kitaaluma.

Hivi karibuni ameandika kingine The BIG PICTURE akieleza pamoja na mambo mengine namna ambavyo wazazi wanaweza kuwalea wanao katika mazingira ya kitaaluma, na jinsi ambavyo jamii yaweza kuondoa tofauti zao za rangi na matabaka ili kujenga jamii moja yenye lengo kuu moja –kujiletea mafanikio.

Mtu huyu kanivutia kwa namna anavyoishi kiafrika afrika japokuwa hakuzaliwa katika bara hili. Utafikiri alisoma makala ya Ndesanjo kuhusu umuhimu wa majina ya kikwetu -watoto wake wote kawapa majina yanayoonyesha uafrika hasa. Vilevile kanivutia namna alivyo na mtizamo wa kijamii kuliko ule wa kibinafsi hasa anapojibu swali, kufanikiwa katika maisha ni kupi?

Nakumbuka kununua kitabu cha kwanza cha bwana huyu nikiwa kidato cha pili. Pamoja na kunichukulia muda wangu mwingi kilinisaidia sana na kunijengea tabia ya kujisomea vitabu. Nimewashauri vijana wengi wa shule kuvisoma vitabu vyake, na wengi wameona faida kubwa kupitia mandiko ya Mwafrika mwenzetu huyu.

Maoni

  1. Huyu jamaa kweli ni kiboko.Hivi Tanzania tunajinsi yoyote ya kufuatilia watanzania wenzetu ambao tunaweza kujisifia na kujivunia kwa vithibitisho vya michango yao katika jamii?Namaanisha kitu similar na Tobblacks lakini hapa ikawa top Tanzanians.Maana ni mara nyingi tunawajua wanasiasa tu.

    JibuFuta
  2. Kitururu, Tatizo ni kwamba watu wa nyanja nyingine, zisizo za kisiasa hawabebi sana vichwa vya habari katika vyombo vya habari. Mwanasiasa ataandikwa sana ahta kama hakuna cha maana alichokisema. Watu wengine inakuwa ngumu kukonga vichwa vya habari katika vyombo hivyo vya uongo kama anavyopenda kuviita Ndesanjo.

    Umefika wakati tukawa na utaratibu wa Top Tanzanias kuwatangaza watu wanaotoa mchango mkubwa katika jamii.

    JibuFuta
  3. naam hii blogu ni nzuri sana, hongera....tujivunie kiswahili.

    Blogu yangu ni http://mswahili-jared.blogspot.com

    baadaye.

    jared

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Uislamu ulianza lini?