Je, Shule za Bweni Zinafaa kwa Malezi ya Watoto Wadogo?

PICHA: SOS Schools


Ongezeko kubwa la shule za bweni kwa watoto wadogo ni kiashiria kimoja wapo cha mabadiliko ya kijamii yanayoendelea kuathiri desturi za malezi. Pamoja na changamoto zake, mzazi anapofanya maamuzi ya kumpeleka mwanae shule ya bweni huamini anafanya hivyo kwa faida ya mtoto.


Mazingira ya nyumbani yanaposhindwa kufikia matarajio aliyonayo mzazi kwa mwanae, kitaaluma kwa mfano, mzazi hutafuta ufumbuzi kupitia shule ya bweni.

Pia, wakati mwingine shule ya bweni huwa ni jitihada za mzazi kumlinda mtoto na changamoto za kifamilia. Wazazi wanapokosa muda wa kutosha kumwangalia mtoto au hata pale wanapokuwa na mgogoro wanaofikiri unaweza kumwathiri mtoto, wanaweza kufikiri kumpeleka mtoto bweni kwa lengo la kumnusuru.

Hata hivyo, wapo pia wazazi wanaoamua kuwapeleka watoto shule za bweni kwa kuwa wamechoka na kile wanachokiita ‘usumbufu’ wa watoto kuwa nyumbani. Shule ya bweni, kwa maana hiyo, ni jitihada za kupunguza makelele nyumbani.

Lakini je, watoto wadogo wanaowahishwa kupata huduma za bweni wanapata malezi yanayolingana na mazingira ya nyumbani? Je, mazingira ya bweni yanawasaidia kujifunza vizuri zaidi kuliko nyumbani?
                                                                                   

Dhana ya ujifunzaji

Jamii imekuwa ikiamini kuwa kujifunza kwa mtoto kunaanzia pale mtoto anapofundishwa maarifa yanayoweza kupimwa kwa mitihani. Tunayachukulia maarifa hayo kwa uzito kwa imani kwamba maisha ya mtoto yanategemea eneo moja la ufahamu wa mambo. Dhana hii, hata hivyo, si sahihi. Ukuaji na maisha ya mtoto kwa ujumla yanategemea maarifa yote anayoyafyonza mtoto kutoka kwenye mazingira yake.

Ili maarifa hayo yawe na msaada kwa mtoto, ni lazima yaweze kugusa maeneo yote muhimu ya maisha ya mtoto. Kwa mfano, mtoto lazima afundishwe maadili, mahusiano yake na watu, masuala ya kiroho/kiimani na stadi za maisha. Mtoto anayejengwa katika haya kwa pamoja, anakuwa na utu ndani yake unaoweza kumwongoza kuwa mtu timamu anayejiheshimu na kuwaheshimu watu wengine. Mtoto anayewekewa msisitizo kwenye eneo moja la ukuaji, hawezi kuwa binadamu timamu.


Nafasi ya ukaribu wa kifamilia

Ukuaji wa jumla wa mtoto unategemeana na mfungamano wa kimahusiano anaoujenga na watu wake wa karibu. Familia ndiyo mahali pekee ambapo mtoto anaweza kupata watu wanaoweza kumwelewa na kujali maendeleo yake kuliko mahali kwingine kokote.

Ukaribu unaopatikana katika familia unamjengea mtoto utulivu wa nafsi. Kule kujua anazungukwa na watu wanaoaminika, kunamjengea hali ya kujiamini. Katika mazingira haya, ya ukaribu wa familia, mtoto anakuwa kwenye nafasi nzuri ya kuiga tunu za maisha kupitia maisha wanayoishi wazazi wake.

Mtoto anaponyang’anywa fursa hii ya kujifunza maisha katika familia yake mwenyewe, anakosa msingi muhimu wa maisha. Kumlazimisha mtoto kujitegemea kabla ya wakati wake, ni kumfungulia milango mingi ya watu wengine kuwekeza mambo ambayo wakati mwingine yanakinzana na matarajio ya mzazi mwenyewe.


Hali ya malezi shuleni

Mwaka 2014 nilitembelea shule kadhaa za msingi za bweni hapa nchini. Lengo lilikuwa kuchunguza ikiwa mazingira ya kimalezi katika shule hizi yanaweza kulinganishwa na malezi yanayopatikana katika familia. Vigezo vya malezi nilivyovitazama vilikuwa ni pamoja na ukaribu baina ya watu wazima na watoto, uangalizi na kiwango cha udhibiti kwa watoto, kutaja kwa uchache.

Katika shule kadhaa, watoto walinipa ushuhuda wa kusikitisha. Wengi wao walionekana wazi kukosa fursa ya kuwasiliana na walezi wao. Nakumbuka mtoto mmoja wa miaka sita alilalamika, “Sijaonana na mama tangu amenileta shule. Nipelekee kwa mama!” Hakuwa peke yake. Watoto wengi hasa wa darasa la kwanza walionekana kuwa wanyonge nilipowauliza mambo yanayowakumbusha nyumbani.

Walezi nao walinisimulia namna wanavyopata shida kuwatuliza watoto hasa mwanzoni mwa muhula. Mmoja wao aliniambia, “Kipindi cha mwanzo wanapoletwa hapa, huwa inasikitisha sana. Usiku hawalali wanalia kurudi nyumbani. Kuna wengine wanafungashaga mizigo yao usiku  wakidai kurudi nyumbani. Inasikitisha sana kwa kweli. Lakini baada ya muda huwa wanazoea na kuchangamka kama wenzao wakubwa.”


Wastani wa uwiano wa mlezi na watoto ulikuwa mlezi mmoja anayeangalia watoto kati ya 50 na 100. Hii ni idadi kubwa. Nilimwuliza mlezi mmoja anawezaje kuwahudumia watoto wote hao? “Ni changamoto kubwa. Jioni wengi wao wanakuwa wanadeka na kulia lia. Kila mmoja anataka nimsikilize. Ninachofanya naanza na wale wadogo wenye shida kubwa. Wengine inabidi wanasubiri.”

Ukaribu kati ya mlezi na mtoto ni hitaji la msingi. Ukaribu huu unapokosekana unamfanya mtoto ajisikie kutengwa. Mtoto anayehisi mlezi anampuuza hupoteza hali ya kujiamini. Hata hivyo, mtoto anayekosa kujiamini wakati mwingine hujenga tabia fulani za kujihami kama alivyoniambia mtoto mmoja wa darasa la pili:

“Kukaa na baba na mama ni mambo ya kitoto,” anacheka na kuendelea, “Ukishakuwa mkubwa kama mimi unaachana na wazazi unatafuta maisha yako.” Lugha kama hii ni mfano mzuri wa kujihami. Mtoto huyu amepoteza thamani ya mahusiano na familia yake. Ufahamu wake umeamua kuwapotezea wazazi ili kupooza maumivu ya kuishi mbali na nyumbani.

Uangalizi hafifu

Nilitaka kujua namna watoto wa bweni wanavyolala. “Tunawachanganya kwa umri,” aliniambia mlezi mmoja na kuendelea, “Wale wa darasa la kwanza tunawachanganya na wale wakubwa ili waangaliane.”

Pamoja na nia njema ya kufanya hivyo, utaratibu huu unaibua changamoto nyingine. Watoto wadogo huwachukulia wale wakubwa kama mfano wa namna ya kuishi. Inapotokea wale wakubwa wametoka kwenye familia zenye desturi tofauti, inakuwa rahisi kwa wale wadogo kuiga tabia zisizofaa.

Pia, katika baadhi ya shule yapo matukio ya wanafunzi wakubwa kuwafanyia wadogo zao vitendo viovu. Wanatumia ukubwa wao kuwanyanyasa watoto wadogo wasio na ubavu wa kuwakatalia.

Nilizungumza na mzazi mmoja kujua kama kuna tabia zozote mwanae anayesoma bweni anazionesha. “Huyu wa kwangu kwa kweli yuko vizuri. Sijaona shida kubwa. Lakini kuna hii tabia ya matusi. Wakati anaondoka kwenda shule hakuwa na kawaida ya kutukana. Nimeona akirudi anatukana wenzake.”

Uwezekano wa mtoto kujifunza tabia mbaya zaidi ya hizi anazozitaja mzazi huyu ni mkubwa. Watoto wadogo wanaotoka kwenye familia tofauti wanapochanganywa hujikuta hawana namna nyingine zaidi ya kufundishana chochote kwa sababu hakuna mtu mzima anayefuatilia kinachoendelea.


INAENDELEA

Maoni

  1. Thanks Nakuelewa sana KWA makala zako uzidi Kutumika kwa Jamii na Mungu akupe nguvu zaidi@stephen Mligo

    JibuFuta
  2. Thanks Nakuelewa sana KWA makala zako uzidi Kutumika kwa Jamii na Mungu akupe nguvu zaidi@stephen Mligo

    JibuFuta
  3. Binafsi naona wazazi tunakwepa majukumu watoto wanatakiwa kulelewa na wazazi hadi walau wamalize darasa la 7 ndipo wajiunge na shule za bweni. Hapo kidogo mtoto anajielewa shule nyingi za bweni hazina uwezo wa kuwafuatilia watoto kwa karibu hasa pale wanapougua hata kugundulika ni kazi.

    JibuFuta
  4. Asante sana kwa maoni mazuri. Shukrani kwa kuwa wadau muhimu wa blogu yetu.

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Uislamu ulianza lini?

Pay $900? I quit blogging