Watoto Wagomvi, Wasumbufu na Wenye Utukutu katika Umri wa Miezi 0 – 36

Tangu tumeanza mfululizo huu, tumejaribu kuonesha namna tabia za mtoto zinavyohusishwa na malezi ya mzazi kuliko vinasaba. Kwa ujumla tumeona kile anachokifanya mtoto ni matokeo ya kufikiwa au kutokufikiwa kwa matarajio yake. Katika makala haya tunaangalia kundi la watoto wenye tabia za ugomvi, utukutu, ukaidi na usumbufu na kuona namna mazingira ya kimalezi yanavyochangia hali hii.

Hawajiamini na hawamwamini yeyote
Kwa ujumla hawa ni watoto ambao hawaoneshi shauku wala sababu ya kutafuta ukaribu na mzazi. Ni watoto ambao tunaweza kusema wamekulia katika mazingira magumu ya kimalezi. Badala ya wazazi wao kuwasaidia kufikia matarajio yao kama watoto, ni wao ndio wanaotumika kama ngao ya wazazi kuficha au kutatua matatizo yao. Badala ya mzazi kuwa chanzo cha mtoto kujisikia usalama, kinyume chake kinatokea. Mzazi anakuwa chanzo cha hofu, mashaka, wasiwasi na hasira.  

Inavyokuwa ni kwamba mtoto anapokwenda kwa mzazi kwa matarajio ya kutulizwa, anajikuta anapuuzwa, anaadhibiwa, anakemewa, anatishiwa na hata kudhalilishwa. Mazingira ya hofu yanajengeka. Njia pekee ya kujihami ni mtoto ‘kumpotezea’ mzazi na kuongeza umbali. Maana yake ni kwamba, hakuna anachoweza kukifanya mtoto kwa mzazi wake kinachoweza kurejesha ukaribu na upendo anaoutarajia. Kila anachokifanya kinaongeza hofu na hali ya kutokujiamini.

Mtoto anakuwa mwoga, anakata tamaa na kuvunjika moyo. Anapoteza imani kwake yeye mwenyewe na kwa wengine. Imani kwake inakwisha kwa sababu anajiona kama mtu aliyekataliwa na kushindwa kumfanya mzazi wake ampende. Hisia hizo humfanya pia amwone mzazi kama mtu asiyeaminika, mkatili, asiyejali, anayetisha na asiyefaa kuwa karibu naye.

Athari kwa mtoto
Katika kipindi cha miezi sita, mtoto wa kundi hili haonekani kuwa na furaha. Uso huoonesha wasiwasi na hofu na hulia lia muda mwingi shauri ya uchungu na kujiona amepuuzwa. Tabia yake akiwa na watu haitabiriki sana katika kipindi hiki ingawa hofu na wasiwasi vinatawala maisha yake. Anaweza kuogopa baadhi ya watu hasa anaojua hawamjali. Wakati mwingine anaweza kuwa na tabia ya kuwang’ang’ania watu fulani fulani anaohisi wanaweza kumpenda.

Mtoto anayekulia katka mazingira magumu Picha: who.int
Anapoachwa na mzazi wake wakati mwingine halii na hana wasiwasi ingawa yapo mazingira anaweza kuwa na tabia ya kulia. Kutokulia ni mafanikio ya jitihada zake za kumpotezea mzazi ambaye kwa ujumla haonekani kuwa mzazi anayejali. Mzazi anaporudi, mtoto huwa hana habari ingawa wakati mwingine huweza kuonesha jitihada za kutambua ujio wa mzazi.

Anapofikia miaka mitatu, sura ya ugomvi huwa bayana. Ni mgomvi anapocheza na mara zote huonekana kufurahia maumivu ya wenzake. Haonekani kuwa na huruma wenzake wanapolia na uso wake hauna uchangamfu wa kawaida kwa watoto wa umri wake. Anaonekana ni mpole lakini kwa hakika ni maumivu yanamfanya awe na moyo uliozizima. Hutumia ugomvi au hasira kama kinga ya kuficha hisia kwamba yeye ndio tatizo. 

Wasiwasi na hofu humfaya ashindwe kujifunza vizuri kama watoto wengine wote wa makundi mengine. Badala ya kujifunza, hutumia muda mwingi kupambana na wenzake ili kujisikie nafuu moyoni. Wakati mwingine anapokutana na watoto ‘rafiki’ wasioendekeza ugomvi, huweza kuwa na tabia ya kuficha hisia zake za ghadhabu na kisasi asichokijua kwa kujaribu kuonesha tabia njema usoni. Hata hivyo, ni mwepesi mno wa kupandwa jazba yanapotokea mazingira ya kumfanya aonekane dhalili. 

Matatizo yanaanzia kwa mzazi mwenyewe
Tafiti zinazonesha hali hii hutokea zaidi watoto wanapolelewa na wazazi waliowahi kukumbwa na matatizo mazito katika maisha yao. Ingawa si wazazi wote wenye historia nzito huwa na malezi ya namna hii,  hata hivyo kuishi na visasi, hasira na uchungu usioshughulikiwa kunaongeza uwezekano wa malezi ya namna hii. 

Mzazi aliyewahi kuachika/kutelekezwa/kudhalilishwa/kukataliwa na mtu muhimu kwenye maisha yake na bado angali akiombolezea hali hiyo, anaweza kuingia kundi hili. Anaweza kuwa mzazi aliyeishi kwenye mateso ya namna fulani katika utoto wake au aliyekumbana na matatizo ya udhalilishaji na hajaweza kusamehe bado. Hali kama hizi huwafanya wazazi kama hawa hujikuta wakilipiza kisasi kwa wengine bila wao wenyewe kutambua. Kisasi hicho kinaweza kuhamia kwa watoto wao wenyewe.

Shauri ya kuwa na visasi mioyoni mwao huwa na tabia ya kuadhibu watoto hali wakiwa na hasira. Wengine huwatukana watoto matusi mazito. Tafiti zinaonesha kwamba asilimia 80 ya watoto wa kundi hili, wanalelewa na wazazi wanaotumia adhabu kali na matusi, hali inayoweza kutafsiriwa na mtoto kama kukataliwa na kudharauliwa. 

Kadhalika, wazazi wenye tabia ya ulevi uliopindukia, wanaotumia pombe kama namna ya kusahau matatizo yanayowakabili. Unywaji wa pombe unapopita kiasi huambatana na ‘kurukwa na akili’, hali inayoweza kusababisha mzazi huyu kuonesha tabia ambazo kwa hali ya kawaida asingezionesha mbele ya mtoto.

Sambamba na hao, tabia ya ubabe na matumizi ya nguvu kwa watu wengine katika mazingira ambayo mtoto anashuhudia huchangia tatizo. Mzazi mwenye tabia ya kupigana, kumtukana na hata kumdhalilisha mwenzi wake mbele ya macho ya mtoto hujenga hofu katika moyo wa mtoto hata kama zipo jitihada za kumwonesha mtoto upendo. Mtoto anayekulia mzingira haya hukua akiamini hayo ndio maisha na huweza kuiga tabia hiyo.

Kwa ujumla tunaweza kusema, tabia ya ujeuri, ugomvi na utukutu kwa kiasi kikubwa huanzia kwa wazazi wanaoishi na matatizo yasiyotatuliwa. Matatizo haya huwafanya washindwe kutambua uhusiano wa makosa yao na maisha ya mtoto. Matokeo yake ni watoto wenyewe kuanza kujibebesha mzigo kwamba tatizo ni wao. 

Hata hivyo, mzazi mwenye makovu ya kihisia moyoni anaweza kabisa kuwa na upendo kwa mwanae. Wapo wazazi ambao pamoja na kuwa na uchungu mkubwa moyoni wameweza kuwatumia watoto kama namna ya kupata faraja.  Wazazi hawa wametumia malezi kama namna ya kushughulikia matatizo yao kwa kuwakinga watoto na yaliyowapata wao. Matokeo yao wamekuza watoto ‘rafiki’ kama tulivyoona kwenye kundi la kwanza. Maana yake ni kwamba, kupitia kipindi kigumu katika maisha si lazima kuathiri malezi yako. Unaweza kabisa kukuza watoto wema kama ukitambua na kufanyia kazi kile kinachohitajikakwa makuzi na malezi ya mwanao.
Inaendelea

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Pay $900? I quit blogging

Uislamu ulianza lini?